Picha: http://www.magic4walls.com

Mwandishi: Mtoto wa Katama

Purukushani za kutafuta picha za mwisho katika ‘albamu’ kuu kuu iliyochakaa. Khamisi hangependa kuacha ushahidi wowote nyuma kwa insani yeyote yule. Juu katika kabati la mamake alilipiga macho albamu lile, lilokuwa limejaa picha lukuki zake pamoja na za ahli zake. Bila kusita alipanda kwenye kiti kidogo na kudakia kwenye upande mmoja wa kabati huku akining’inia kama ngedere. Mle juu ya kabati kulikuwa na vumbi si haba, tandu za buibui zilitapakaa kote. Alikitia mkono kwenye magorogoro yale na kulivuta albamu lile. Chafya zilimparamia kwa ghafla! Himidi nazo zikaja nyingi tu! Kwa sababu ya vumbi lile. Kombamwiko na panya nao walikuwa kila mtu roho mkononi walitawanyika kila hayawani akikimbilia maskani mapya, laity wangalijua kuwa ‘operesheni’ nzima ilikuwa ni juu ya ‘albamu’ wala wasingejitia tumbo joto. Khamisi alijiachilia chini na kukita kwa kishindo pu! Aliguna ki bebeeru beehh! kutokana na maumivu kwenye visigino.

 

Baada ya kutulia kidogo na maumivu kupungua, alivuta pumzi nzito na kufungua kurasa ya kwanza ya albamu lile. Kumbukumbu zilifurika akilini, moyoni alijiambia “kumbe mamangu naye alikuwa mrembo wakati wake”, “hivisasa tumempata amechoka maskini ya mungu” alijisuta. Akafikiria zile taabu mamake anapitia na mchana ule, kuzungusha bamia na dagaa gengeni siku kutwa na muda mwengine kuambulia patupu. Khamisi alishawahi kumshawishi mamake mara nyingi tu! Kuachana na biashara ile. Waswahili washam’maliza kwa kumkopa, naye Mola kampa roho ya huruma kukataa kukopesha haezi na kudai hela yake ni mzito ajabu. Kipindi kimoja Khamisi alimkaripia mamake zeituni, ‘ibilisi’ alikuwa amemjaa pomoni haskii la mwadhini, aliamua leo ni leo.”Hivi mama wewe mbona kisirani sana, hela ya mamangu utalipa lini” alifoka. Mamake Khamisi alposkia purukushani zile ukumbini, alitoka chumbani kwa kasi na kufululiza hadi alipokuwa amesimama Khamisi. “Achana naye Khamisi nakuomba mwanangu, mlaani shetani, kama biashara ni yangu” alimsihi Khamisi. Kidogo Khamisi mori ukashuka na kumwachilia mamake zeituni baada ya kubembelezwa. Lakini naye akaapa kutoingilia tena masuala ya biashara za mamake na wala mamake asimuhusishe na lolote. Yote hayo akiyafikiria akajiona kweli kakosa, zile tabu zote mamake alizopitia ilikuwa ni kwa ajili yake na ndunguze. Na alijutia siku ile kumkana mbele ya mamake zeituni, lakini yashamwagika hakuna la zaidi ila kujirudia na kuisuta nafsi yake.

 

Zile picha za mamake zilimnogea kwa kipindi kidogo mara “Ngo! ngo! Ngo!” zilisikika kelele za mlango ukigongwa na kumshtua kutoka kwenye lindi la mawazo. Khamisi,kwa sekunde kadhaa alibaki kimya akijaribu kusikiliza tena ikiwa ni kweli mlango ulikuwa ukigongwa au alikuwa akiweweseka.kwa dakika kadhaa alikuwa bado amesimama akiendelea kusikiliza lakini hakusikia chochote,taratibu alishusha pumzi na kuendelea kuangalia albamu lakini kabla hajaendelea kufungua kurasa nyingine shuka alisikia mlango ukigongwa tena na wakati huu mlango ulikuwa ukigongwa kwa nguvu na sekunde chache kukawa kimya tena.Kwa mara nyingne Khamisi aliamka taratibu na kuingiwa na wasiwasi kidogo kwani mudaule hakuwa anamtarajia mtu yeyote. Alijaribu kufikiria atakuwa nani huyu? Moyoni alijiuliza bila kupata jibu mwafaka. Akaamua kujikokota polepole, alipofika karibu na bawaba, aliskia mtu akishusha pumzi nzito nzito.

 

Mara kidogo akaita “Khamisi, Khamisi ehhh! Upoo”, Khamisi si muda akaifahamu sauti ile na kujibu “ Nipo babu, haya nipe la mwafaka umefuatia nini?, maana niko bize kiasi”. “ Fungua kwanza nikueleze, usikuwe hivyo” Lipopo akanena. Khamisi akazubaa kidogo na kufungua mlango, akamuangalia lipopo jinsi alivyokuwa anateremkwa na jasho, akajua hapa kuna habari za muhimu ila hakupendelea masahibu zake kumfuatia nyumbani kwao. Alipendelea kumaliza shughuli zote wakiwa kijiweni au nje ya nyumba. Lipopo alipojaribu kujitokomeza chumbani, Khamisi alimzuia na kifua na kumnyoshea kidole akiashiria wakazungumzie nje. Lipopo hakuwa na la zaidi ila kufuata maagizo na kutangulia huku Khamisi akimfuatia nyuma. “ Hebu niambie lililokuleta na mbio zote hivyo ni lipi haswa?” Khamisi aliuliza…

Author

A freelance writer, journalist, poet and blogger venturing mainly in social and community issues, study and analysis of behaviour and life, and the plight of the under-dogs in the society. 'I feed on human stories.'

Write A Comment