Tag

Maisha


Browsing

Mwandishi: Lali Mohamed

Picha: http://www.travelstart.co.za

Mwana dunia ni jando, njia njema ifuata,
Uvumilie vishindo, yote yatayokukuta,
Chako usitupe kando, qadari hutoifuta,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Ya duniani menendo, mengi ni kama karata,
Kisha kuna na maondo, mitihani kukupata,
Ela sifanye mtindo, wa kwako ukamkata,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

La kukata ni uvundo, fikiri ukilimata,
Vionye vyako vitendo, kila moyo ukiteta,
Kukata hakuna mwendo, kisha kuunga utata,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Jizoeze kwa ukindo, kilo chako kukamata,
Ufuate na mwenendo, wa kutatua matata,
Pa ufa sishike tindo, mwanya ukaufuata,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Sitilie mno pondo, la ukuruba kufuta,
Wala usifanye pendo, kutangaza umekata,
Kukata kuna mafundo, kinyongo kijapo kita,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Tesi zi kama vimondo, na hisani huzifuta,
Nyoyo zikabaki pindo, kila mmoja asuta,
Ujapo wafanya wendo, mafundoni utajuta,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Mwandishi: Sultan Karama Maji Male (kero)

 

Niipoketi  katika  fuo ya bahari nikitafakari kuhusu mambo  mengi fikra ilipita katika Kina kirefu cha bahari giza totoro likiwa limetanda Kulia na kushoto, mbele na  nyuma,  juu na chini. Ama Kwa hakika maisha ni mti mkavu.

Nilijaribu kuleta tafakuri langu Kwa mara  nyengine  tena Kwa jambo lengine. Aaah wahenga  nadhani hawakukosea waliposema  Umasikini ni uvundo. Hichi  ndicho  chanzo cha donda ndugu lililo nisibu fuadini mwangu ila  ni hadithi  ya muda  mwengine. Hebu turudi katika  maukifu yangu nilioko. Nilisikia kuwa  Mungu hamtupi mja wake. Labda msemo huu ndio ulionipa ari ya kuendelea kurusha ngumi na mateke kujitetea katika vita hivi Kati yangu na huu ulimwengu uliojaa na udhalimu.

Nguvu Za kurusha ngumi kujitetea sinazo tena na sababu Za kujitetea zilitoweka zamani. Kila mtu ana  Mungu au kama vijana wa kileo wanavyosema “Mungu Tu” . Nilienusha  mikono juu na kumuomba  Maulana assuage wingu hili ambalo kunyesha  halinyeshi ubaridi halileti na njia ya kwenda  mbele limeziba.

Nikiwa katika maombi hayo nagundua tundu inayotia maji katika chombo changu. Wingu limeziba mpaka upepo na tanga imeraruka. Abiria wako katika hali ya kukata  tamaa na baadhi yao tayari wamesharuka katika bahari  tayari kuliwa na papa kuliko kuweka imani kwangu na kunipa moyo wa matumaini. Kwa mbali naona Abiria mmoja ameanza kuchoka. Anataka kuachilia ila anaogopa bahari isije kumsoza. Moyo unanivunjika na maini kunikatika Kwani  sikudhani  abiria  yule atafikia  katika  hali ya kutaka kushuka katika jahazi langu. Huyu ni yule abiria  aliekuwa  mcheshi  mwanzo mwa  safari na kuwa na mazungumzo  ya mtu mwenye upeo Wa mbali. Kwani  ni nini  kilichobadilika  Kando na hali ya hewa?  Nikiwa katika maswali hayo ndio naona kipote kidogo sana kinachonitia moyo.

“Nahodha kaza  demani” ndio maneno  ya kikundi kidogo kilichobaki nami. “Usijali tutafika Manda. ”  Japo maneno yao yanatia hima kuendelea  na safari ila ni muhali kuendelea.  Nguvu zimenishia wala sitaki kuwaonesha kuwa nimekata tamaa. Ila ukweli ni  kwamba  ninasubiri  tu amri yake jalali kwani  mawimbi huzidi kuwa mazito na chombo kinazama  taratibu  sijui hali ya hewa itageuka au nitapata Wa kuniauni? Yako mengi ya kutafakari ila Wa kutafakari na mimi yuko?  Ni  nani  atakaeamua kunisaidia katika safari hii ya shida na Adhabu? Aso na wake ana  Mungu.