Mwandishi: Lali Mohamed

Picha: http://www.travelstart.co.za

Mwana dunia ni jando, njia njema ifuata,
Uvumilie vishindo, yote yatayokukuta,
Chako usitupe kando, qadari hutoifuta,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Ya duniani menendo, mengi ni kama karata,
Kisha kuna na maondo, mitihani kukupata,
Ela sifanye mtindo, wa kwako ukamkata,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

La kukata ni uvundo, fikiri ukilimata,
Vionye vyako vitendo, kila moyo ukiteta,
Kukata hakuna mwendo, kisha kuunga utata,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Jizoeze kwa ukindo, kilo chako kukamata,
Ufuate na mwenendo, wa kutatua matata,
Pa ufa sishike tindo, mwanya ukaufuata,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Sitilie mno pondo, la ukuruba kufuta,
Wala usifanye pendo, kutangaza umekata,
Kukata kuna mafundo, kinyongo kijapo kita,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Tesi zi kama vimondo, na hisani huzifuta,
Nyoyo zikabaki pindo, kila mmoja asuta,
Ujapo wafanya wendo, mafundoni utajuta,
Usijifunze kukata, ukiunga huwa fundo.

Author

A freelance writer, journalist, poet and blogger venturing mainly in social and community issues, study and analysis of behaviour and life, and the plight of the under-dogs in the society. 'I feed on human stories.'

Write A Comment