Mwandishi: Sultan Karama Maji Male (kero)
Niipoketi katika fuo ya bahari nikitafakari kuhusu mambo mengi fikra ilipita katika Kina kirefu cha bahari giza totoro likiwa limetanda Kulia na kushoto, mbele na nyuma, juu na chini. Ama Kwa hakika maisha ni mti mkavu.
Nilijaribu kuleta tafakuri langu Kwa mara nyengine tena Kwa jambo lengine. Aaah wahenga nadhani hawakukosea waliposema Umasikini ni uvundo. Hichi ndicho chanzo cha donda ndugu lililo nisibu fuadini mwangu ila ni hadithi ya muda mwengine. Hebu turudi katika maukifu yangu nilioko. Nilisikia kuwa Mungu hamtupi mja wake. Labda msemo huu ndio ulionipa ari ya kuendelea kurusha ngumi na mateke kujitetea katika vita hivi Kati yangu na huu ulimwengu uliojaa na udhalimu.
Nguvu Za kurusha ngumi kujitetea sinazo tena na sababu Za kujitetea zilitoweka zamani. Kila mtu ana Mungu au kama vijana wa kileo wanavyosema “Mungu Tu” . Nilienusha mikono juu na kumuomba Maulana assuage wingu hili ambalo kunyesha halinyeshi ubaridi halileti na njia ya kwenda mbele limeziba.
Nikiwa katika maombi hayo nagundua tundu inayotia maji katika chombo changu. Wingu limeziba mpaka upepo na tanga imeraruka. Abiria wako katika hali ya kukata tamaa na baadhi yao tayari wamesharuka katika bahari tayari kuliwa na papa kuliko kuweka imani kwangu na kunipa moyo wa matumaini. Kwa mbali naona Abiria mmoja ameanza kuchoka. Anataka kuachilia ila anaogopa bahari isije kumsoza. Moyo unanivunjika na maini kunikatika Kwani sikudhani abiria yule atafikia katika hali ya kutaka kushuka katika jahazi langu. Huyu ni yule abiria aliekuwa mcheshi mwanzo mwa safari na kuwa na mazungumzo ya mtu mwenye upeo Wa mbali. Kwani ni nini kilichobadilika Kando na hali ya hewa? Nikiwa katika maswali hayo ndio naona kipote kidogo sana kinachonitia moyo.
“Nahodha kaza demani” ndio maneno ya kikundi kidogo kilichobaki nami. “Usijali tutafika Manda. ” Japo maneno yao yanatia hima kuendelea na safari ila ni muhali kuendelea. Nguvu zimenishia wala sitaki kuwaonesha kuwa nimekata tamaa. Ila ukweli ni kwamba ninasubiri tu amri yake jalali kwani mawimbi huzidi kuwa mazito na chombo kinazama taratibu sijui hali ya hewa itageuka au nitapata Wa kuniauni? Yako mengi ya kutafakari ila Wa kutafakari na mimi yuko? Ni nani atakaeamua kunisaidia katika safari hii ya shida na Adhabu? Aso na wake ana Mungu.