Mwandishi: Jotham Mwashighadi
Picha ni kwa hisani ya Youtube.com
Niko ziara ardhini, waridi kukutafutia
kalala huko nyikani, nikateswa na vidudu
nalialia jangwani, uso umesawajika
Elewa langu waridi, maua ni nadra mno
Nimegaga upwani, kusaka mkate mweupe
Viganja vimatesoni, mtulinga umepindika
Kutumwa nimetumika, nikutunze ubavu
Elewa langu waridi, maua ni nadra mno
Nilimilki bustani, ilosheheni uturi
Rangi za kububujika, mandhari ya paradiso
Nyuni na vikembe, walihani tenzi za upendo
Elewa langu waridi, maua ni nadra mno
Majira yana misimu, misimu ina vipindi
Naitamani shairi, tuitie chachu majini
Mboni tuangaliane, hapa tu tutafaraji
Elewa langu waridi, maua ni nadra mno
Kibaba cha didimia, kwa miale ya msimu
Siha zetu tabaani, chumi na uwekezaji
Nibuni vipi wapenzi, msimu wa furaha?
Elewa langu waridi, maua ni nadra mno
Nidhinishe kipepeo, japo bustani limetota
Jipambe kwa hi na wanja, nami kwa tabasamu
Tuogelee hewani, tukuze chuki ya halaiki
Elewa langu waridi, maua ni nadra mno
Wazistahili nyota, za mji wa mbinguni
Sasa udhuru naomba,nikupe ua lining’inialo kama popo
vumilivu kama mbavu, Korosho na tundale jekundu
Elewa langu waridi, maua ni nadra mno
Mbegu ni zao kamili, kanju ua la bakshishi
manjano au nyekundu, ishara ya hisia za joto
Korosho ina rotuba, hifadhiwa hadi kesho
Kanju ua la nyauka, hudonwa si kesho
Tukitua kipepeo, pokea korosho na uale