Author

Jotham Mwashighadi


Browsing

Utu  mkakosa, mkanivunja uti

Mkanilainisha kama poda

Nikawa chakula cha mchwa

Mkanisahau

Navuma gizani

 

Majira yakaficha weusi wenu

Mkasihi jumuia isahau

Ikajumuika

Mkasali kwa sauti gugumizi

Mkanifukia

 

Kisu kilichonisafirisha  gizani

Keki chapakua, msimu mtamu tena

Kwa wepesi viuno mwakata

Kinyume cha  rai za nafsi

Mwangwi wa bezo wavuma gizani

 

Mbaya mimi siko. Mnafuraha?

Mwizi mimi siko. Akiba mnazo?

Simo idadini. Shibe mnayo?

Wageni hawalaumiwi

Utu  haba ni giza.

 

Burdani ni ua la sumu

Laficha ukweli leo, kesho halimo

Uongo hauna starehe

Kwa miyayo tu, mawimbi yataibua

Uongo mlioficha miongoni.

 

Navuma gizani, sikio hamna

Vitenge mwajikwatua kote nyajani

Pambio zateleza vinywani

Hatimaye kukaripia ndugu adui

Ndimi. Vumi. Pepo

 

Ngoma ni tamu, waichezao hawachoki

Wana kiu cha matunda, rangi si hoja

Yawe kijani au manjano

nyayo nyekundu kwa vumbi

zameremeta kama mshale wa moto.

 

Hatima yangu mwaitamani?

Maficho kwa stesheni

Na chini ya msalaba

Hatimaye kufanywa

Kuni. Kaa. jivu baridi

 

Je? kama sanda yastiri

Mbona mkanifukia?

Mwaficha nyuso kwa matendo yenu?

Fumbueni macho muone jua

Tiba ni toba

 

Mtapona lini?

Nasikia nyayo juu ya kifua

Mwakimbiza nani leo?

Jua likitua, mtacheka.

Kesho mtalia.

 

Shehena ya wivu kinywani

Wakongwe bado wala chumvi

Ajabu!

 

  1. Hili ni shairi huru.
  2. Ritifaa ni sanaa ambayo inahusisha mtu aliyekufa, akiwasiliana na waliohai
  3. Picha kwa hisani ya http://walterastrada.com. Inaonyesha mtu mwenye hamaki kipindi cha 2007/2008,ambapo kulitokea ghasia baada ya upigaji kura

Powered by WordPress