Picha: https://www.123rf.com/photo
KE Gif Ge 468X60
BARUA KWA RAFIKI(1)
Rafiki ninapotuma waraka huu,sina uhakika kama utakufikia.huenda uliniblock. Lakini nadhani huezi kuniblock maana mara ya mwisho nilikuacha na simu ya kabambe.Lakini kama ulipata simu ya ndoto zako yenye kila kitu mpaka nailcutter,basi labda umeniblock.Haidhuru.
Barua hii naiandika nikiwa hapa hotelini na kikombe cha kahawa.kama ni zamani na wewe ungekua hapa na kikombe chako cha chai.lakini ulinitenga. Hatuongei tena. Maskani ulibadilisha. Hunipigii simu kama zamani kunicheka timu yangu imefungwa.yule binti uliyekuwa ukinipigania nimpate usiku na mchana,nilimpata.lakini hauwezi hata kumuita shemeji. SABABU YA SIASA. Sababu tulitofautiana kimawazo. Sababu hatuko chama kimoja. Lakini rafiki mbona hawa tunaowapigia kura wanalala hoteli moja,magari yao yamefanana. Kwanini sisi tutengane rafiki?
Nimeishiwa na bundle kama kawaida yangu,na hapa nilipo hakuna WIFI. Nitarudi tuongee nikikopa credit. Rafiki yangu mpendwa,ni mimi rafikiyo wa tangu utotoni. Mapacha tusiofanana.
BARUA KWA RAFIKI(2)
Rafiki naskia umemuoa mchumba wako wa miaka mingi.Hongera.Nawatakia kila la kheri.Japo ulivunja ahadi yako ya mimi kua chandama(bestman) wako.
Rafiki ulisema ukijaaliwa watoto utawapa majina mazuri zaidi duniani. Lakini mbona rafiki mbona unaita watoto wa wenzako majina mabaya mabaya? Mbwa,mjinga,mshenzi,hayawani.Na mengine yasosemeka wala kuandikika? KWA SABABU YA SIASA.
Rafiki samahani,najua sikulishi,sikuvishi wala sikubabaishi
Lakini unapoteza muelekeo.
Samahani rafiki,shemeji yako ananiita.
Wacha nikamsikize.
Nisije nikampoteza kama yule mwengine.
BARUA KWA RAFIKI(3)
Rafiki,kama ungekua shabiki wa nyimbo za Diamond kama mimi,ningesema umeamua ukae kimya kama huyo bingwa.Lakini wewe ni shabiki wa King Kiba. Kibao chenu cha mwisho ni “Aje”
Lakini mbona kwetu pia huji?
Ama ukaniita mimi nikaja na rafiki zangu?
SABABU YA SIASA.
Rafiki,basi angalau na sisi tutoe nyimbo inayoitwa “Chuki”tupate pesa kama Diamond na Kiba.
Lakini kuekeana chuki kwa sababu ya siasa hatupati kitu.
Alafu hii barua muoneshe na shemeji,yeye ni team Diamond.mpe namba zangu angalau nimrushie hii nyimbo mpya.
BARUA KWA RAFIKI(4)
Hongera rafiki.Naskia umenunua gari la ndoto zako,WISH.Natamani na mimi nilijue nambari ya usajili(number plate)kama ninavyojua nambari za usajili za Gavana,Senator na Mbunge wetu lakini haiwezekani.Angalau kama ungetimiza ahadi yako ya kuandika mstari wa shairi langu ‘SIRI JAPO SIO SANDA,ZANGU NITAZIKWA NAZO’ nyuma ya gari lako,pia ningeliona ningelifahamu.Lakini pia hivyo hauwezi.SABABU YA SIASA
Siasa ndo itakayokufanya unipite mimi nikitembea,huku umefunga vioo,na tunaishi mtaa mmoja.
Rafiki kama hio chuki itaniwezesha na mimi kununua gari pia kama lako,maana ndo gari la ndoto zangu pia,basi ingekua afadhali.Lakini hio chuki inatubomoa,haitujengi.
Nimefika kwenye hiki kichochoro hatari,nisije nikaporwa kikebe changu cha simu,ni hiki hiki tangu uliponiacha…
#SIASASICHUKI
#TAHADHARI
#SimulizizaMalenga001