Mwandishi: Lali Mohamed
Picha: http://s.ngm.com/
Pani kalamu watani, na waraka baidhia
Ninukuu ya huzuni, yanayosibu dhuria
Hunipa shaki moyoni, kashika tama kalia
Wana wasio hatia, roho zao tafarani.
Roho zao masikini, wana wachanga Syria
Wamehiliki machoni, wazazi waangalia
Jitimai na huzuni, Rabi wasahilishia
Wana wasio hatia, roho zao tafarani
Walokabili jamani, ni jambo la kutishia
Huvamiwa mitaani, wengi wakaangamia
Hata walo majumbani, mikononi kuwafia
Wana wasio hatia, roho zao tafarani.
Wameikosa amani, fazaa zimewangia
Wamengia adhabuni, hawatambui kadhia
Na majumba yako chini, hawana pa kuingia
Wana wasio hatia, roho zao tafarani
Imewatoka makini, hawakai kutulia
Kutwa kucha mafichoni, adui kumkimbia
Gafula viambizoni, bomu huwarepukia
Wana wasio hatia, roho zao tafarani
Wamekosa tumaini, amani kuwarudia
Wameita wahisani, bila ya kuitikia
Wamebakia gizani, hatari hata kulia
Wana wasio hatia, roho zao tafarani
Watoto ni kosa gani, hujuma kuwafanyia?
Kuwabakisha njiani, wazazi wamejifia
Wakala vya majaani, bila tiba na afia
Wana wasio hatia, roho zao tafarani
Lanikeketa maini, kila nikifikiria
Huwaza wana vitani, huwaje tukawatia?
Walakini ifaeni, imepofuka dunia
Wana wasio hatia, roho zao tafarani
Tamati nilobaini, si jambo la kuridhia
Tusiate miswalani, dua kuwakumbukia
Awaizishe Manani, irudi tena Syria
Wana wasio hatia, roho zao tafarani