Tag

albamu


Browsing

Mwandishi: Mtoto wa Katama

Picha: http://www.magic4walls.com

 

Kwa mara nyingne Khamisi aliamka taratibu na kuingiwa na wasiwasi kidogo kwani mudaule hakuwa anamtarajia mtu yeyote. Alijaribu kufikiria atakuwa nani huyu? Moyoni alijiuliza bila kupata jibu mwafaka. Akaamua kujikokota polepole, alipofika karibu na bawaba, aliskia mtu akishusha pumzi nzito nzito. Mara kidogo akaita “Khamisi, Khamisi ehhh! Upoo”, Khamisi si muda akaifahamu sauti ile na kujibu “ Nipo babu, haya nipe la mwafaka umefuatia nini?, maana niko bize kiasi”. “ Fungua kwanza nikueleze, usikuwe hivyo” Lipopo akanena. Khamisi akazubaa kidogo na kufungua mlango, akamuangalia lipopo jinsi alivyokuwa anateremkwa na jasho, akajua hapa kuna habari za muhimu ila hakupendelea masahibu zake kumfuatia nyumbani kwao. Alipendelea kumaliza shughuli zote wakiwa kijiweni au nje ya nyumba. Lipopo alipojaribu kujitokomeza chumbani, Khamisi alimzuia na kifua na kumnyoshea kidole akiashiria wakazungumzie nje. Lipopo hakuwa na la zaidi ila kufuata maagizo na kutangulia huku Khamisi akimfuatia nyuma.

 

“ Hebu niambie lililokuleta na mbio zote hivyo ni lipi haswa?” Khamisi aliuliza. “Usikuwe hivyo yakhe, mbona una hasira” akajibu Lipopo kwa kunyeng’enyea.” Mi hapa nimekuja na mazuri, Bw.Salimu atuhitaji tukamuone habari ndiyo hiyo” Lipopo akamalizia akiongea huku akitabasamu. Khamisi akamuangalia Lipopo toka juu mpaka chini, kana kwamba alikuwa anampima hivi katika mizani flani hivi. Akautazama uso wa Lipopo na kisha akatikisa kichwa baada ya kufanya dadisi zake na kuenusha mikono juu na kuleta dua “Ewe Mola! Uliye juu, mpe mja wako huyu shughli ya kufanya na wepesi wa kuongea” na kucheka kwa dhihaka. “Kumbe we ovyo! Hivi muda wote uliopoteza kumbe maneno yalikuwa ni haya, kama ingekuwa umenitaarifu pale mlangoni ulipogonga kungeharibika lipi? na tuonane hiyo jioni” Khamisi akafoka bila kusubiri jibu la Lipopo na alimuacha akiongea peke yake na kugeuka mbio mbio na kuingia nyumbani kwao. “Watu wengine wapuuzi kweli, wanafaa makofi chap! chap!” alijisemea moyoni. Alipoingia chumbani, alijipiga kichwa na kidole chake mara kadhaa na kupiga macho huku na kule mpaka akaliona albamu, muda wote lilikuwa lipo kitandani na hakudiriki kuangalia kwa makini, kisha akatabasamu kwa kujiona bwege kweli. Ikawa anaendelea na kulifungua huku akicheka ovyo ovyo, picha zake za utotoni zimleletea furaha na kumbukumbu tamu sana. Kwenye picha moja aliona kitoto kidogo, puani akitokwa na kamasi na magwanda yake ya kuchanika. “Kweli huyu ni mimi lo! Haiwezekani huu mzaha sasa, labda ni mdogo wangu Idrissa, itakuwa Idrissa tu!” alijaribu kujisemeza. Lakini alipokodoa macho vizuri na kuangalia ile picha kwa umakinifu aligundua kuwa ni yeye. Pichani mtoto alikuwa na alama ya ngozi nyeusi katika mguu wake na hofu zake zote zikawa kweli. Hakupendezwa na picha ile kamwe, ye keshakuwa barobaro sasa na ndevu zilishaanza kuota, tena zilimea kwa ajabu sana. Zilikuwa zimetapakaa kwenye kidevu kwa vifungu vifungu kama matuta kwenye shamba la mkonge. Alishajaribu mbinu nyingi kuzifanya ziote vizuri, huyu huyu Lipopo aliwahi kumwambia apake asali iliyochemshwa na kuchanganywa na haba soda(habbat sawda) kwenye kidevu chote. Alifuata masharti kama alivyoambiwa na mwendani wake wa karibu. Lakini matokeo hayakuwa mazuri, hata siku ilikuwa haijaisha Khamisi alipata mwasho wa ajabu na kuishilia kujikuna kwa wiki mbili mfululizo, mkuno ulileta yale mapele magumu kidevu kizima. Kwa wiki mbili nzima alibaki ndani kwa ndani tu kama mwari aliyeletewa posa na mtoto wa Sultani. Alidiriki kutoka usiku tena mara moja moja kwa sababu ya shughuli za kimsingi. Tena alitembea kwa tahadhari nyingi sana alinyatanyata kwenye vichochoro kwa staili ya kimgambo ili asiwahi kupishana na watu wanaomjua. Lakini waswahili wanasema siku utakayokwenda uchi ndiyo siku utakayokutana na mkweo na naam!

 

Usiku mmoja katika mishe mishe zake za kuenda kununua chapatti mitaa ya ndani usiku, baada ya kukata vichochoro vitatu viwili ghafla bin vuu! mchumba wake Zeituni alitokea kwenye chochoro. Khamisi alipunguza hatua, na kumuangalia vizuri mtu aliyekuwa anakuja kwenye upande mwengine wa kichochoro kama kweli ndiye aliyekuwa anamdhania, baada ya kugundua kuwa alikuwa Zeituni, polepole alipiga kona na kutaka kurudi alipokuwa anatokea. Kweli ile siku anayokufa nyani miti yote huteleza, mara tu bila mpangilio paka wawili shume  waliokuwa wanakimbizana wakatokea kwenye upande wa uchochoro aliokuwa Khamisi anaregea nao. Toba ya Ilahi! Khamisi alikuwa muoga wa paka ajaabu bora hata angekutana na nyoka. Yeye na paka ni mbingu na ardhi. Aliamua kubarutika mbio upande aliokuwa anaokuja nao Zeituni na kumpiga kumbo mchumba wake huku akitokomea kwenye giza bila hata kushikwa na wasiwasi wa kuangalia nyuma. Kwa hasira Khamisi alichukua ile picha ya mtoto na kuichanachana vipande vipande na kuitafuna, hakuweza kukubali kuwa mtoto yule mchafu na kamasi zake kuwa alikuwa ni yeye na cha zaidi alichukia kwa kuwa yakhe. Hakuelewa kwanini watu wengine walijaaliwa mali na wengine kunyimwa.

 

Mara Khamisi alitulia kwa ghafla baada ya kufungua kurasa nyengine ya albamu lile, akasita kwa muda, macho yakawa mazito na machozi kuanza kumlengalenga. Akawa baridi na ukiwa ukamtawala kwa ghafla, akajiona mnyonge ajaabu na kufunga albamu na baadaye kulifungua tena. Picha iliyofuatia ilikuwa ni ya marehemu babake. Ni miaka kumi imepita tangu kumpoteza babake katika ajali ya barabarani iliyonaswa na vyombo vya habari karibia vyote. Taarifa za kifo cha babake zilimpa mshtuko zaidi nina yake aliyekuwa mtegemezi zaidi, hakujua angeanzia. Baba Khamisi ndiye alikuwa anatarazaki pekee yake. Tena Baba Khamisi shughli zake zilikuwa nadhif kabisa, alisifika kwa kufanya adala baina ya watu na zaidi kwenye shughuli zake za kila siku. Lakini kinaya kilikuwa ni madhila na unyanyasaji mamake Khamisi aliyopitia kutokana na nduguze mumewe. Haya yote Khamisi aliyaelewa kabisaa na alikuwa ameweka nadhiri kitambo ya kupanga kisasi…