Tag

mahaba

Browsing

 LEO TANENA KWELI

Mwandishi: Fafi

Picha: http://www.thedigestonline.com/

Leo tanena kweli, yaliyo mwangu moyoni

Siezi kustahimili, niyafiche kwanini?

Enyi wazazi wawili, nisikilizeni kwa makini

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

Mumetupeka shuleni, chuo kikuu hususani

Twashukuru kwa yakini, ila tupo matatani

Mumetutia mitihanini, hisia zetu kutozibaini

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

Hakika huku chuoni, ni wake kwa waume ndani

Twajizuia chanzo dini, si rahisi mnavyodhani

Tutafunga tusizini, ila tutafunga mpaka lini?

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

Mnaogopa ya duniani, walasio ya akherani

Miaka yetu ya ishirini, damu iko motoni

Leo niko masomoni, kesho nina mwana tumboni

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

Muhimu kuwaozesha, wale waloridhiana

Ikiwa huba lawakimbisha, msikae kuwakana

Msidhani hawana hisia, si magogo wala spana

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

Ni vyema kuwaangalia, japo uwezo hawana

Wawezapo watajisaidia, muhimu kuvumiliana

Tueleweni nawalilia, tumridhishe wetu Rabbana

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

Tamati nimefikia, hoja yangu nimewaachia

Ni mengi ya kusikitikia, hayasemeki nawaambia

Lau mutazingatia, dhambi mtatupunguzia

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?