Picha: http://images.fineartamerica.com/images-medium-large/a-father-and-sons-hands-min-suh.jpg
Mwandishi: Sultan Karama Maji Male (kero)
Bismillahi jaliya, muumba wa binadamu,
Kwako wewe nalekeya, naanza kutakalamu,
mwanangu namuusiya, ya dini kuyafahamu,
Nakuidhi ya buneyya, wasia ulo muhimu.
Si shiriki ya buneyya, nafusi kujidhumu,
Hana kuffu na sawiya, ni yeye pweke karimu,
Muumba wa samawiya, bila umudi kukimu,
Nakuidhi ya buneyya, wasia ulo muhimu.
Wazazi kuwatendeya, hisani yenye kudumu,
Kwa kina kuzingatiya, tumboni kwa wako ummu,
Kwa wahani aliliya, kubeba lako jukumu,
Nakuidhi ya buneyya, wasia ulo muhimu.
Kwa juhudi zisikiya, zao wazazi hukumu,
Illa zikikosa ndiya, na kukhalifu ilimu,
Ruhusa nakupatiya, kufwata hakulazimu,
Nakuidhi ya buneyya, wasia ulo muhimu.
Jema ukijifanyiya, la khardali fahamu,
na ovu kulipapiya, la haba au timamu,
Mola atakuleteya, siku hiyo ya qiyamu,
Nakuidhi ya buneyya, wasia ulo muhimu.
Yalo mema hadithiya, na sala zako zikimu,
Misiba kuvumuliya, maovu kuyashutumu,
Mambo yote azimiya, muelekee rahimu,
Nakuidhi ya buneyya, wasia ulo muhimu.
Jauri kujisikiya, usifanye kwa kaumu,
Na mwendo ukitembeya, maringo yasitakimu,
Mola anawachukiya, fakhuri wenye hujumu,
Nakuidhi ya buneyya, wasia ulo muhimu.
La mwisho nakuambiya, sauti yako khadhimu,
Ni ya nikari twabiya, himari yake isimu,
Hifadhi nalo kwambiya, usije kunilaumu,
Nakuidhi ya buneyya, wasia ulo muhimu.
Tag
Browsing