Mwandishi: Sultan Karama
Picha: http://0.tqn.com/
Anavyojua yeye, magari yakigongana yote huharibika na safari husimama kwa muda. Lakini mbona la mwenzake liliondoka palepale? Mbona halikuhitaji ukarabati? Ama ilikuwa ajali ya kupangwa? Haya ndio baadhi tu ya maswali yaliokuwa yakimgonga kichwani. Aliketi kitandani akaangua kicheko. Aliucheka moyo wake kwa kuvunjwa mara kwa mara lakini haukomi. Mara akanuna. Aucheke moyo wake au ajicheke yeye?
Alikuwa kinyume na jina lake. Sudi hakuwa na bahati Katika ulingo wa mapenzi . Alibaki kusikia kutoka kwa simulizi za watu utamu wa mapenzi, ila kwake hayakuwa tofauti na subili. Alimeza funda la mate mazito kwa uchungu mno. Afanye nini aupoteze uchungu uliomvaa? Kipi afanye ili moyo uwe huru? Nani wa kumsikiza amlilie? Alimtafuta wa kumuauni na kumpa faraja wakati ule akose.
Alimkumbuka mpenziwe Fatuma Baraka na ahadi teletele walizowekeana. Alikumbuka nyakati nyingi alivyojitahidi kumfurahisha nana ila jitihada haziondoi kudura. Alihisi kusalitiwa na mtu aliemuamini. Sasa ni yupi wa kuaminiwa tena? Ama kweli kutendwa ni kubaya. Alitamani ardhi ipasuke immeze mzima mzima. Alihisi huu ndio mwisho wa uhai ila alijipa matumaini “Mungu huleta sahau .” Ila swali ibuka ni : lini itakuja sahau? Lini atamsahau kimwana? Vipi aweze kumsahau Fatuma wakati hata kichupa cha marashu kilimkubusha mwanamke yule wa shani?
Alikitupa kichupa kile cha marashi maana kila akikinusa alimkumbuka asietaka kumkumbuka. Kwenda kununua chengine pia alishindwa,maana hakuna wa kumpeleka kumsaidia kuchagua kama zamani. Hii ni tamati ya kila kitu katika aushi. Alijitupa kitandani na kutuliza bongo lake kwa makini ili apate usingizi lakini lepe alilolitarajia halikuja ila mawazo ya bimkubwa yalimjia moja baada ya nyengine. “Sie huyu alieniahidi kutoniacha?” “Huyu kijana ‘A’ ni nani kwani na ni kipi kilichomvutia nyongo mkalia ini? Ama kweli Audi sina sudi “
Kawaida ya moyo ukifikiwa na mazito huongea kwa kutoa machozi lakini moyo wake ulikuwa bubu uliongea kwa Ishara. Ghafla akatabasamu. Bahari ina samaki wengi tafi, tangu,una,kiboma an wengine wengi ila yeye alipenda simsim pamoja na udogo wao. Lakini walipomdunga kwa miba yao alisusia samaki, alisusia mpaka pweza wasio na mwiba. Alibughudhiwa kwa mandhari yao ila alijiona huru kabisa.
Baada ya kurudishiwa moyo wake jioni ile,hakurudi nyumbani. Alipitia kwa mpiga chapa, akatoa nakala kadha wa kadha za moyo wake ili Kama atapenda tena atapeana nakala hatopeana moyo wake.