Tag

Swahili fiction


Browsing

Mwandishi: Mtoto Wa Katama

Mara Khamisi alitulia kwa ghafla baada ya kufungua kurasa nyengine ya albamu lile, akasita kwa muda, macho yakawa mazito na machozi kuanza kumlengalenga. Akawa baridi na ukiwa ukamtawala kwa ghafla, akajiona mnyonge ajaabu na kufunga albamu na baadaye kulifungua tena. Picha iliyofuatia ilikuwa ni ya marehemu babake. Ni miaka kumi imepita tangu kumpoteza babake katika ajali ya barabarani iliyonaswa na vyombo vya habari karibia vyote. Taarifa za kifo cha babake zilimpa mshtuko zaidi nina yake aliyekuwa mtegemezi zaidi, hakujua angeanzia. Baba Khamisi ndiye alikuwa anatarazaki pekee yake. Tena Baba Khamisi shughli zake zilikuwa nadhif kabisa, alisifika kwa kufanya adala baina ya watu na zaidi kwenye shughuli zake za kila siku. Lakini kinaya kilikuwa ni madhila na unyanyasaji mamake Khamisi aliyopitia kutokana na nduguze mumewe. Haya yote Khamisi aliyaelewa kabisaa na alikuwa ameweka nadhiri kitambo ya kupanga kisasi.

Njia mbili za machozi zilibubujika kama mtoto mdogo, kile ambacho hakuelewa zaidi ni watu alowaita ami zake kuwageuka bila hata huruma na kuwaonyesha unyama wa aina ya mwisho, akajiuliza hivi kweli damu ina uzito wowote? Anaikumbuka vizuri ile siku aliposhuka eda mamake kulikuwa na timbwili la aina yake. Ami zake walikuja na kupiga wanawake kisaramgambo waliokuja kumfariji mamake Khamisi,  walijaza nyumba ya kina Khamisi na umati ili kushuhudia tafarani waliyoileta ya kugombea hati miliki za ardhi za marehemu babake. Mama kwa unyonge akaona yote ya nini haya alijionea aepukane na balaa zote na kuwaachia waondoke na stakabadhi hizo muhimu karatasi. Zegere lote hilo likitokea ndio mwanzo kuanza kubaleghe na angejiletea ‘laana’ tu! Bure kwa kuingililia mgogoro ule wa watu wazima, lake likawa ni jicho. Albamu lile lilizidi  kumkumbusha mavi ya kale, kweli hayaachi kunuka! Fikra mpya zikamjia “mimi nishakuwa rijali sasa, na nina haki ya kurithi alichoacha marehemu babangu” alijinong’oneza.

Ari ya kulipiza kisasi ikazidi kumtawala, machozi nayo yakazidi kumdondoka, roho nayo ikafungama na kujisokota na machungu ya miaka yote ile. Mwili nao ukawa unatetema na kusisimka, utasema kapigiwa ngoma za kula nyama mfu za wachawi kilingeni. Akaanza kuguna na kunguruma kama simba, sasa mwili ulizidi kutetemeka utasema zezeta yaani kiufupi mwili mzima ulikuwa chini ya ‘milki’ mpya, mara ghafla akaanza kupiga nduru “ Uwiiii Leo nauwa babu, natamani harufu ya damu sana” akapayuka payuka huku mate yakimdondoka. Yallahu yalamu, mizimu ya kwao ilikuwa ishaenuka, nani atakayemrudisha chini? Wenyewe husema yakwao yakienuka hata kwa lifti hayashuki. Aliinama na kuchochomeza mkono katika mojawapo ya tendegu la kitanda, baada ya kupapasa alichomoa sime Enhe! Kwa kweli kilikuwa kimeumana aisee! Pyuu! Aliponyoka tu utadhani panya aliyejinasua katika mtego baada ya mrefu wa kukata tamaa na maisha , hata mlango aliuacha wazi ng’waa wote alisahau mle ndani kulikuwa na ‘uhai’ wao wote, japo vitu vilivyokuwa ndani havikuwa na thamani sana lakini ndivyo vilivyowatunza na urathi waliobaki nao pekee. Haswa haswa dhahabu za mamake mara nyingi alishayeyusha vipande kwa sonara ili kukidhi mahitaji ya nyumbani. Mara nyingi aliepuka mialiko ya harusi za uswahilini kwa kukosa herini na bangili, aliogopa kuwa ‘topiki’ ya mtaani, sababu ya kuyeyusha vito vyake ni, wakati mwengine huja kipindi ikawa hana chochote kabsaa sasa na inambidi akate pua ili aunge wajihi. Wajihi ambao ni akina Khamisi na ndunguze, wajihi ambao Khamisi alikuwa anaenda kuuharibu licha ya matatizo aliyopitia mamake mzazi.

“ Uwiiii! Jamani huyo chungeni ana silaha. Atamwaga damu” kamsa zilisikika kutoka kila sehemu, kila mtu alikimbia njia yake kuokoa roho yake,barabara ikaleta taswira ya Rwanda watutsi wakiwakimbia wahutu, wazungu wenyewe wangesema ‘running for your dear life’. Wale waliokuwa barabarani wakiuza bidhaa zao waliziacha na kutokomea wasijulikane wanakokimbilia ililkuwa ni tafarani moja kwa mbili, wengine walijikung’waa na kuanguka, mmoja alijipata akiogelea katika sufuria la uji wa ngano moto, Lo! Alishaharibia watu kiburudisho chao cha muda wa baada ya alasiri bora hata angeangukia kwengine na kujifia. Hivi watu wote wakapati wapi sharubati ya kushukishia viazi vya karai. Ila mchezo kando yale matukio yaliyokuwa yakiendelea pale yalikuwa ni ya mguu niponye, utasema kila mtu anakimbilia hukumu yake ya siku ya kiyama baada ya parapanda kupigwa na malaika Israfil . Mara Khamisi akapita mbio katika barabara ile na kushika uchochoro mwengine, jambo hilo lilimtia wasiwasi zaidi huyo aliyemtangulia katika kichochoro hiko, kosa lake kubwa kuaachana na wenzake na kuamua kukimbia peke yake na wenziwe kuchukua njia nyengine. Sasa hapo ndio muda wa kujilaani na kujijutua kuachana na wenzio maana waswahili husema kifo cha wengi ni harusi, hivi yahkhe leo anajiona akitolewa roho pekee yake. “Kesha pagawa! Wallahi ameshakuwa chizi, lakini ole wake akili zikimarudia atatulipa biashara zetu sote” nyuma sauti ziliskika zikilaani kwa hasira. Lakini Khamisi hakuwa na shida nao, ni umbea wao tu uliowachongea, yaani hivi ukiona mtu akija mbio na panga na nyinyi eti mnaamua kukimbia….eti ehh?  Swali hilo. Yaani mnakurupuka tu ovyoo! Na kujijeruhi na kusababisha hasara biashara zenu…kwani hamjawahi kuona wamasaai wakizunguka na sime zao viunoni? Na wala hamjawahi kukimbia, hivi leo mnamuonea ajabu Khamisi. Khamisi naye yeye alikuwa anakimbizwa na ajenda zake, mbio zote hizo alikuwa akieleke akwa ami zake…………………

 

Powered by WordPress