Tag

Waislamu


Browsing

Picha: http://missionislam.com/

Mwandishi: Fafi

Uislamu ni dini ya imani, yenye msingi wa Quran na Sunnah ambayo ni maneno na vitendo vya mtume (S.A.W). Nguzo za uislamu ni mfumo wa maisha ya muislamu. Nazo ni shahada, swala, utoaji wa zakah(kuwasaidia wenye dhiki), kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhan na kuhiji Makkah japo mara moja kwa mwenye uwezo. Ni dini yenye wafuasi wengi na sana sana hutambulika kwa jinsi waislamu wanavyofuata dini yao.

Wanazuoni wa sharia ya kiislamu walisema kwamba kuna mambo sita ya sita ambayo mwanadamu anafaa kuyalinda vyovyote iwezekanavyo. Kwanza ni maisha. Unapochukua maisha umeokoa maisha, ndipo dini ikaamrisha kuuliwa kwa atakaye muuwa mwenzake yani qisas. Mathalan anapopanga mtu kuuwa kisha akahofia adhabu ile, hivyo basi dini imeokoa maisha ya watu wawili na kadhalika. Siri ya pili ni mali. Mali ni jambo la kuthaminiwa sana ndio maana ni sharia kwa anaedaiwa kulipa deni hilo na unapoiba mali ya mtu anafaa kukatwa mkono. Ya tatu nayo ni hadhi yani “izzag”. Mwanadamu anatakiwa alinde hadhi yake na pia heshima yake. Ndio sababu ya kuwekwa sharia ya kumpiga mwenye kuzini au kumpiga kwa mawe hadi kufa kwa wale waliokuwa kwenye ndoa.

Siri ya nne nayo ni akili. Muislamu anafaa kukaa na akili zake timamu kama alivyoumbwa na mwenyezi Mungu mtukufu. Ndipo kukaharamishwa pombe na mihadarati yote. Muislamu hafai kuwa na uraibu wa kitu chochote ila isipokuwa ni halali na hakina madhara kwake. Mtume Muhammad rehema na Amani zimshukie yeye amesema, “mwenye kufa ilhali yupo katika hali ya uraibu basi amekufa kifo cha mshirikina”.

Siri ya tano ni kizazi. Ni jukumu letu kulinda kizazi na kujenga undugu. Mathalan, kiislamu mke wa mtu hafai kumfungulia mwanamme yeyote kuingia kwake ikiwa mume wake hayuko. Mtume wetu asema “shemeji ni kifo” kwa sababu anatangamana na mkeo na mwisho anaweza kukusaliti. Siri ya mwisho ni dini. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema kwenye kitabu chake tukufu katika sura ya nane aya ya thelathini na tisa,

“na wapigeni vita mpaka kuwe hakuna fitna na iwe dini ya Allah peke yake. Lakini wakiacha hakika mwenyezi Mungu anayaona wanayoyatenda”. Kwa hiyo ni lazima tulinde dini yetu.

Tukiangazia hali ya uislamu duniani tunapata kuna madiliko chungu mzima ambayo yamejitokeza. Uislamu tuliokuwa nayo leo sio kama vile zamani ambapo kila mahali palikuwa shwari na dini yenyewe ilikuwa inanawiri. Kila siku zinavyopita na maendeleo kukithiri ndivyo waislamu haswa vijana wanavyokumbana na changamoto. Kama tunavyojua, hiki kipindi cha ujana, kuanzia miaka kumi na sita hadi thelathini na tano ndipo homoni za mwanadamu zinakuwa moto. Hapa ndipo utakuta kijana anakutwa na kila aina ya majanga. Alisema mtume wa mwenyezi Mungu (S.A.W) miongoni mwa makundi saba ya watu ambao watakuwa chini ya kivuli cha mwenyezi siku ya kiyama ni kijana ambaye moyo wake umeambatana na msikiti. Kijana ambaye anashinda msikitini akimtukuza Allah na kutenda ibada akitafuta ridhaa zake. Tunapoangazia haya yote ndipo tunapotanabahi ya kwamba kijana ana nafasi kubwa sana katika mujtama’a wa uislamu na maisha kwa ujumla. Hivyo basi ni muhimu tuangazie kwa kina zile changamoto zinazowakumba vijana na zile sukuhu amabazo tutapendekeza.

Naam, changamoto zeneyewe zinatofautiana kulingana na sehemu anapoishi yule kijana. Wale wanaoishi katika nchi zinazotawaliwa kwa mfumo wa kiislamu changamoto zao zina nafuu tukilinganisha na wale wanaishi katika nchi zinazotawaliwa kwa mifumo mingine kama vile demokrasia na mingineyo.

Changamoto ya kwanza kabisa ambayo ambayo ningependa kuizungumzia ni swala la Elimu. Elimu naweza kusema ni kama msumeno, hukata mbele na nyuma. Mathalan, ina kochokocho na manufaa yake mingi pia. Mfumo wa elimu yetu ulivyo unaweza kupoteza watoto kuanzia umri mdogo wanapojiunga na shule za chekea. Kwa mfano kuna nadharia ambayo vijana wetu wanafundishwa katika somo la historia ambayo ni potofu sana. Nadharia kama ile inayowafunza wanafunzi kwamba wanadamu wanatoka na kizazi cha kima ni moja wapo ambayo inapotosha watoto. Elimu kama hii inaanza kumchanganya mwanafunzi na kuanza kushuku vitu vingi vya dini ambavyo sio sawa. Wako wazazi ambao wanapeleka watoto wao katika shule za dini zingine kama vile wakatoliki wanaambiwa kwamba Nabii Issa ni mwana wa Mungu. Ukienda kama marekani utapata watoto wanaambiwa kwamba kila mtu ana uhuru wa kufanya kila jambo analotaka. Wanafunzwa kwamba maumbile yako tofauti, utapata watu wa jinsia moja wanafanya mapenzi. Haya yote yanatokana na athari ya masomo ambayo wanayapata katika shule hizi. Dini iko na msimamo mkali kuhusu jambo hili. Lakini watoto wanakua na mambo haya kwa akili halafu inafikia muda inakuwa ngumu kumbadilisha mtu. Mwenyezi Mungu anasema kwenye kitabu kitukufu kwenye sura ya saba aya ya themanini na moja,

“nyinyi manaowaendea wanaume kwa kuwa mnawatamani badala ya wanawake! Ama nyinyi ni watu wafujaji”.

Katika wakati wa maswahaba, walikuwa wakichoma na kuwaacha pasi na kuwaswalia hata janazah wanaofanya tendo hili ovu. Je kama tumewafunza watoto wetu na kuwapa elimu ya dini wangejihusisha na tabia kama hizi?

Ama kwa upande wa pili, elimu pia ni nguzo katika mambo mengi, tumeamrishwa tutafute elimu. Elimu husaidia katika mambo chungumzima kujikimu kimaisha. Suluhisho kwa jambo hili ni kwa wazazi wahakikishe watoto wao wanapata elimu iliyo sahihi. Na hali zisizoepukika inawalazimu wawe wakihimiza wanana wao kujua dini itakayowasaidia leo na kesho akhera.

Ama changamoto ya pili ni mihadarati na madawa ya kulevya. Jambo hili sana sana husababiswa na shinikizo vijana wanapokuwa hawana kitu cha kufanya na hupata wakati mwingi wa kutangamana na wenziwao walio waislamu na hata wasio waislamu. Vijana na waislamu kwa jumla tuko wa aina mbili. Kuna wale wenye Imani thabiti na wale wenye Imani dhaifu. Wale vijana wenye Imani ya nguvu wanaweza kukataa wanaposhawishiwa kufanya jambo lisilo kuwa la sawa. Ama kwa wale wenye Imani dhaifu wao hujikuta wamefuata wenzao kwenye maasi. Suala la madawa ya kulevya ni suala la kusikitisha sana na linaathiri ulimwengu mzima. La kusikitisha Zaidi ni kwamba hapa kenya, pwani ndio inayoongoza. Tunapoteza vijana wetu wenye akili nzuri. Vijana ambao wangeimarisha dini ya kiislamu pamoja na kuleta maendeleo katika nchi kuichumi, michezo na Nyanja nyinginezo. Suluhisho ya jambo hili ni kuwapa vijana wetu ajira ili wasipate muda wa kukaa mabarazani au maskani kama wanavyoziita sehemu hizo. Tunaweza kuja na miradi tofauti tofauti.

Changamoto ya tatu ni teknolojia. Jambo hili pia ni ndumakuwili kwani faida zake na hasara zinakaribia kuwa sawa. Waswahili wanasema kuwa mgala muuwe na haki yake umpe, hivyo basi ningependa kuanzia na mazuri yaliyoletwa na teknolojia. Dini ya kiisalamu na ulimwengu kwa jumla umeendelea pakubwa kutokana na manufaa yaliyoletwa na teknolojia. Tumeweza kusoma dini kwa mtandao na kufanya utafiti wa kila aina kwa mtandao. Shughuli za nchi pia zimeweza kufanywa kwa wepesi na urahisi na kusababisha maendelea makubwa katika Nyanja mbali mbali kama vile kilimo.

Teknolojia vile vile imeleta maafa mengi sana. Ujumbe wowote kwa mfumo kama vile video, sauti au hata arafa umekuwa mkubwa na rahisi. Jambo hili limefanya vijana kuona picha chafu ambazo zinawaharibu akili. Zinawapotezea muda wao kwa sababu siku hizi vijana wanakesha kwenye mtandao wakifanya upuzi mwingi. Akili zao zinakuwa zimejaa mambo yasiyokuwa na maana. Ndipo ukapata kijana mkubwa wa umri tu lakini akili ya watoto. Hawawezi kukomaa kiakili iwapo mambo wanayoshinda wakifanya ni ya kipumbavu. Imezidisha zina katika jamii, kiasi cha kuwa watu wanazini mpaka hadharani. Pia imevunja ndoa nyingi sana katika jamii ya kiislamu. Vijana wanasasisha kila jambo wanalofanya katika mitandao ya kijamii kama vile “Facebook”,”Twitter” na “Instagram”. Kumekuwa hakuna siri tena. Jambo hili linaweza kusababisha husuda pia. Na jambo lingine katika kusasisha mambo kwenye mtandao ni katika utoaji wa sadaka na zakah. Mtu anatoa zakah na sadaka ambayo ni mambo mazuri lakini anajitangaza kwenye mitandao hii. Hili linapelekea mfumo mzima wa kupeana kwake sadaka na zakah kuwa riyaa. Mtume (S.A.W) anasema “toa kwa mkono wa kulia,wa kushoto usijue.” Mambo mengine kama haya huenda yakatufanya tukose thawabu kwa jinsi tunavyojumuisha vitu. Na huenda zikabadilisha nia yetu zakufanya matendo na tukaishia kufanya mambo visivyo. Suluhisho ya jambo hili ni kuwa tunatakiwa kuwa waangalifu katika kumpokea mgeni huyu. Tujaribu vilivyo kuepukana na fitina iliyomo ndani ya jambo hili. Tutumie kwa mambo yatakayoimarisha dini yetu, kusaidia jamii na ulimwengu kwa jumla.

Changamoto ya nne ni Umoja. Sisi kama waislamu tunatakiwa kuwa wamoja. Tushikamane, tushirikiane na tusaidiane katika mambo yetu ya kila siku. Tutakapo fanya hivi tutakuwa na msimamo bora kabisa na msingi bora wa kimasisha. Tutakuwa kielelezo chema kwa watu wasiokuwa waislamu. Tukiwa pamoja tunaweza kuvutia adinasi lukuki katika dini yetu. Umoja huleta maendeleo, furaha na Amani. Tutaweza kusuluhisha tatizo hili kwa kwa kukubali na kuzifahamu tofauti zetu, na sote tujiangalie kama waislamu na wala sio kutumia makabila kujitambulisha. Hakika kizazaa chengine kipo katika malezi. Tena nasisitiza MALEZI! Asilimia kubwa anavyokuwa kijana husababishwa na malezi yanayotokana na wazazi. Kwanza mzazi anamlea mtoto kwa matusi, kivipi tunataraji mtoto huyo ataongea maneno mazuri akikuwa.

Mtoto anapigwa kama ngoma, mtoto huyo ni mbwa mara kesho ni punda. Kuna wazazi wenye vilma vichafu jamani. Ndipo pale watoto wanakulia vibaya. Pili watoto haswa wale wenye mzazi mmoja, pengine baba pekee au mama. Kuna wale wanaoacha kuwashughulikia wanawao kifedha pindi tu akimuona yule mtoto kakuwa lakini hajapata njia yoyote ya kujikimu kimaisha. Jambo hili ni hatari sana hususan kwa wasichana. Wewe kama mzazi unatarajia mtoto kama yule atoe pesa za kujikimu wapi? Wapo wasichana wengi wanaoathirika na mambo kama haya ndani ya vyuo vikuu. Tukiongea ukweli hapa ni kama yule mzazi anamsukuma yule mtoto aende akaombe. Na ataombea wapi? Mahali penye pesa si kwa wavulana wadogo kama wao bali ni mijibaba yenye pesa zao! Na tukumbuke hakuna vya bure. Ndipo hapo tunaskia flani kapachikwa mimba, mara flani kapata ukimwi. Alafu flani ndio atalaumiwa bila kuzingatia mzizi uliomeesha miba hiyo, ambayo ni wazazi. Sasa ombi langu kwa wazazi kama vile mulivyoanza kuwaangalia watoto wenu walipokuwa wadogo, maadamu mtoto huyo hajapata namna halali ya kupata riziki, ni wajibu kwenu kuwaangalia hata kama ni hicho chako kidogo, mpe! Ataridhia na kutosheka kuliko kumnyima kisha kuletewa majanga nyumbani, waama usipoziba ufa utajenga ukuta. La tatu utapata wazazi ambao hawana uhusiano mwema au wa karibu na watoto wao. Hii inasababisha watoto wajihisi wametengwa, wanakosa ule upendo unaotakikana hivyo basi wanaenda kupenda watu wasio sahihi. Kwa ujumla wazazi wajitahidi waepuke mambo kama haya.

Ama changamoto nyingine ambayo inatukumba ni kuwepo wanazuoni wengi wenye kutofautiana hivyo basi kutuchanganya na kutuacha kwenye mataa. Mathalan ukienda mjini capetown katika nchi ya afrika kusini, wapo wanazuoni wanaoamini kitabu kitukufu cha Quran lakini hawaamini hadith za mtume. Sasa tunashangazwa, kwa sababu tukiangalia suala kama hilo,swala iliteremsha na kutajwa katika Quran lakini idadi ya rakaa tulipata kwa Mtume(S.A.W). kivipi leo tupate wanavyuoni wanaokubali Quran na kukataa Sunnah! Pia hivi majuzi nchini ufaransa walipiga marufuku mavazi ya hijabu na mitandio. Kisha pakatokea mwanachuoni mmoja kutoka sehemu za Azhar na kusema watu wafuate marufu hayo. Sasa wafaransa walianza kuwacheka waislamu kwa kutojielewa. Mtume Muhammad (S.A.W) alisema,

“Ninachohofia Zaidi katika ummah wangu ni wanazuoni dhaif”. Vile vile tofauti katika kufasiri ayah za Quran na hadith zinasababisha vijana kutojielewa. Vijana husikiza khutbah za wanazuoni wengi.

Jambo la ndoa za kulazimishwa ni jingine ambalo linawakumba vijana wa kiisalamu. Hili hutokana na wazazi kuwa na tamaa ya pesa ama mila kwa makabila mengine. Jambo hili sio zuri na ni moja katika sababu kuu zinazosababisha kuongezeka kwa talaka katika jamii. Mwenyezi anasema kwenye Quran katika sura ya wanawake aya ya 19;

“Enyi mlioamini! Si halali kwenu kurithi wanawake pasi na matakwa yao, wala msiwazuie (kuolewa kwa wanaume wengine kwa kuwa hamuwataki) ili mupate kuwanyang’anya baadhi ya zile mlizowapa. Isipokuwa wawe wamefanya uovu uliowazi…..” hadi mwisho wa ayah. Ndoa kama hizi za kulazimishwa haziruhusiwi. Suluhisho ni kwamba wazazi wanapaswa kuacha tabia kama hzi.

Nayo changamoto nyengine ambayo inawakumba vijana na waislamu wengine ni hisia za udhalili. Asilimia kubwa ya waislamu hawajiamini. Hawajiamini kidini na pia mambo mengine ya maana. Tunafaa kutambua kwamba dini yetu ndio ya haki na kila kilichoamrisha na mwenyezi Mungu kina sababu yake, unaweza kuithibitisha kisayansi au pia kimantiki. Uislamu ndio unajali maslahi ya kila mtu. Sisi kama waislamu tunatakiwa tujiamini kidini kwanza kisha mambo yote yatafunguka. Tuondoe shaka kabisa katika akili zetu.

Tatizo jingine kubwa linalotupata ni mazingira ya kazi. Vijana tunakumbwa na fitina nyingi katika kazi zetu. Unyanyasaji wa kijinsia kwa wavulana na wasichana. Sio kazi za uhandisi,sio maofisini,sehemu karibia zote hapakosekai tatizo hili. Ukweli ni kuwa tunaweza kupunguza mambo kama haya kwanza kwa kuhakisha wasichana wamevaa kiheshima na kuwepo mazingira ya kazi ya kuheshimika. Unajua wanaume wana maradhi mengi sana yasiyoeleweka. Itakuwa vyema basi kuhimizana kumcha mola na pia kuheshimiana.

Powered by WordPress