Tag

ndoa


Browsing

Picha: https://pixabay.com

Sikilizeni kwa makini, mwenzenu nipo matatani…
Kwa mkubwa mtihani, ulonipata duniani…
Na nimekita mawazoni, sijui nifanye nini..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?

Mimi ni mke nyumbani, na pia mimi ni mama…
Pili nilikua shuleni, na chuo kikuu kusoma..
Kishida nilisoma jamani, kwa juhudi zake mama..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?

Kwa kupenda Rabana, shahada nikatunikiwa..
Kwa kweli niling’ang’ana, mwishoe nikafanikiwa..
Nikapata wangu bwana, harusi nikafanyiwa..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?

Sasa nipo kwenye ndoa, mume wangu kakatalia
Amelitia kubwa doa, ndoto zangu kutimia…
Nikimweleza huniondoa, hataki kamwe kusikia…
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?

Hataki nifanye kazi, ataka nikae nyumbani..
Kinyume atakavyo mzazi, niwasaidie mashinani..
Hawana kazi wala bazi, na watoto tele nyumbani…
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?

Nina madada nyumbani, bado wapo masomoni..
Kuwasaidia natamani, ila kweli siwezani…
Imenipa tafshani, nakaa bila amani…
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?

Kando na ya nyumbani, ninazo ndoto zengine…
Uhandisi uwanjani, nifanye kama wengine…
Hunichoma roho ndani, nikashindwa nisinene..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?

Nawaomba ushauri, njia ipi nifatilie..
Niende zangu kazini, wazazi wafurahie..
Au nikae nyumbani, mume wangu aridhie..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?

Asanteni.

Mwandishi:Sultan Karama Maji Male (kero)

 

1. Taanda kumswifu, Rabi mola Jalali
Thumma swalatu alifu, zimfikie rasuli
Na swahabaze ashirafu, kina Ali na Bilali
Kuna ubaya gani, kuwaangalia walooana?
2. Japo damu huchemka, tumeamua kutulia
Sio kuwa tunataka, kumuasi Jalia
Ila mambo kadhalika, mangi yanotufikia
Kuna ubaya gani, kuwaangalia walooana?
3. Mwaogopa ya duniani, ndilo la muhimu sana
Hebu pima fikirani, ndo mwamuudhi Rabana
Eti kisa tu chuoni, hatufai kuoana
Kuna ubaya gani, kuwaangalia walooana?
4. Tumechoka kuzini, vijana tumetubia
Tumerudi ibadani, kwa Mola wetu Jalia
Tuoneeni imani, vijana twawalilia
Kuna ubaya gani, kuwaangalia walooana?
5. Na la kuzingatia, hamukosi kwa Rabana
Kwenye kutusaidia, tunapo kwaruzana
Tapungua na udhia, hilo fahamu sana
Kuna ubaya gani, kuwaangalia walooana?
6. Beti sita nimetimu, naweka kalamu chini
Rabi ndiwe ni hakimu, uhukumuo Manani
Vijana tunalaumu, wakutusikiza ni nani?
Kuna ubaya gani, kuwaangalia walooana?

 LEO TANENA KWELI

Mwandishi: Fafi

Picha: http://www.thedigestonline.com/

 

Leo tanena kweli, yaliyo mwangu moyoni

Siezi kustahimili, niyafiche kwanini?

Enyi wazazi wawili, nisikilizeni kwa makini

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

 

Mumetupeka shuleni, chuo kikuu hususani

Twashukuru kwa yakini, ila tupo matatani

Mumetutia mitihanini, hisia zetu kutozibaini

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

 

Hakika huku chuoni, ni wake kwa waume ndani

Twajizuia chanzo dini, si rahisi mnavyodhani

Tutafunga tusizini, ila tutafunga mpaka lini?

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

 

Mnaogopa ya duniani, walasio ya akherani

Miaka yetu ya ishirini, damu iko motoni

Leo niko masomoni, kesho nina mwana tumboni

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

 

Muhimu kuwaozesha, wale waloridhiana

Ikiwa huba lawakimbisha, msikae kuwakana

Msidhani hawana hisia, si magogo wala spana

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

 

Ni vyema kuwaangalia, japo uwezo hawana

Wawezapo watajisaidia, muhimu kuvumiliana

Tueleweni nawalilia, tumridhishe wetu Rabbana

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?

 

Tamati nimefikia, hoja yangu nimewaachia

Ni mengi ya kusikitikia, hayasemeki nawaambia

Lau mutazingatia, dhambi mtatupunguzia

Kuna ubaya gani, kuwaangalia walio oana?