Picha: https://pixabay.com
Sikilizeni kwa makini, mwenzenu nipo matatani…
Kwa mkubwa mtihani, ulonipata duniani…
Na nimekita mawazoni, sijui nifanye nini..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?
Mimi ni mke nyumbani, na pia mimi ni mama…
Pili nilikua shuleni, na chuo kikuu kusoma..
Kishida nilisoma jamani, kwa juhudi zake mama..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?
Kwa kupenda Rabana, shahada nikatunikiwa..
Kwa kweli niling’ang’ana, mwishoe nikafanikiwa..
Nikapata wangu bwana, harusi nikafanyiwa..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?
Sasa nipo kwenye ndoa, mume wangu kakatalia
Amelitia kubwa doa, ndoto zangu kutimia…
Nikimweleza huniondoa, hataki kamwe kusikia…
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?
Hataki nifanye kazi, ataka nikae nyumbani..
Kinyume atakavyo mzazi, niwasaidie mashinani..
Hawana kazi wala bazi, na watoto tele nyumbani…
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?
Nina madada nyumbani, bado wapo masomoni..
Kuwasaidia natamani, ila kweli siwezani…
Imenipa tafshani, nakaa bila amani…
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?
Kando na ya nyumbani, ninazo ndoto zengine…
Uhandisi uwanjani, nifanye kama wengine…
Hunichoma roho ndani, nikashindwa nisinene..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?
Nawaomba ushauri, njia ipi nifatilie..
Niende zangu kazini, wazazi wafurahie..
Au nikae nyumbani, mume wangu aridhie..
Nimefika njia panda, jamani nifate ipi?
Asanteni.