Mwandishi: Mtoto wa Katama

 

“Kesha pagawa! Wallahi ameshakuwa chizi, lakini ole wake akili zikimarudia atatulipa biashara zetu sote” nyuma sauti ziliskika zikilaani kwa hasira. Lakini Khamisi hakuwa na shida nao, ni umbea wao tu uliowachongea, yaani hivi ukiona mtu akija mbio na panga na nyinyi eti mnaamua kukimbia….eti ehh?  Swali hilo. Yaani mnakurupuka tu ovyoo! Na kujijeruhi na kusababisha hasara biashara zenu…kwani hamjawahi kuona wamasaai wakizunguka na sime zao viunoni? Na wala hamjawahi kukimbia, bivi leo mnamuonea ajabu Khamisi. Khamisi naye yeye alikuwa anakimbizwa na ajenda zake, mbio zote hizo alikuwa akielekea kwa ami zake.

 

“Mamake Zeituni hivi umemuona Khamisi!” mamake Khamisi aliuliza kwa mshangao, baada kuona mlango wa chumbani mwake uko wazi na sio jambo la kawaida. “Huyo fedhuli wako bangi zimemparamia! naskia anafukuza watu na mapanga huko nje” akajibu kwa jeuri, “uliskia watu wanazaa na wewe ukazaa! Utakoma this time!” Akazidi kuleta kejeli na kumsazaa mwenziwe “subiri kuitiwa mzoga, maana waja hawatambakisha”.

 

Maneno hayo yalizidi kumkang’anya na kumtia wasiwasi mamake Khamisi hata mwili ukamuisha nguvu na kushindwa kujibu, ila alisimama na kutafakari maneno yale, “hivi kweli anamuongelelea Khamisi ama naye keshapigwa puza”. Maana alimjua mwanawe Khamisi kijana mpole sana hivi leo alfu ulela za kuzunguka na mapanga wapi na wapi na Khamisi. Moja jumlisha moja haikuleta mbili kwake kabisa, aliingia chumbani na kuangalia taswira mle ndani, kile kimya kilichokuwa mle ndani kilikinzana na fikra zake, maana akili yake ilikuwa fikra za ghasi tu. Mboni zake ‘zikaangukia’ kwenye albamu lile, kurasa iliyokuwa wazi ni ya marehemu mumewe. Akasogea na kulichukua albamu lile, akatazama kwa uzuri na makini ile picha utadhani anajaribu kuleta kumbukumbu za kumfahamu aliyekuwa katika picha ile. Wajihi ulikuwa umebadilika teyari! Kiwingu cha majonzi kikampa kivuli, akajifikicha macho na kanga yake aliyokuwa amejitanda mabegani. Akavuta pumzi polepole ya kutuliza kichwa na akafunga albamu lile chap! chap! na kufungua kabati na kutoa kanga nyengine ya kujitanda kichwani, kanda mbili mguuni, akavuta mlango na kutia komeo. Fyuuuup! Na kutoka haraka, kutokomea.

 

Umati ulianza kufurika kwa haraka! Kila mtu aling’ang’ania kupata sehemu nzuri ya kusimama ili kujionea matokeo ya bure. Kweli limbukeni hana siri! kama ibada zingekuwa zinajazwa kwa mtindo huu! wala Mola asingetuletea maafa yeyote na riziki zingekuwa kwa wingi. Wenyewe wanasema uswahilini hakuna dogo, madogo hufanyika uzunguni. Kila anayefika pale alitaka kujua kilichokuwa kinajiri, ila majibu sasa yalitegemea na pahali ulipokuwa umesimamia. Habari zilizotoka kwa ‘wapambe’ waliokuwa mbele ya tukio hazikushahabiana na zile zilizokuwa zikipeperushwa kwa wale waliokuwa nyuma. Kila zilipowafikia waliokuwa nyuma zilikuwa tata zaidi kila mmoja ‘aliongeza chumvi’ kwa kiasi alichokipenda yeye. “Eti naskia kuna jini limeingia mle ndani” mmoja aliropokwa, mwengine akamkata juu kwa juu “sio jini babu ehh! ni joka kubwa limo humo ndani”. Sasa hio ndio ilikuwa hali halisi ya uswahilini, wanahabari wengi walishafutwa kazi kwa kuchukua habari za wanakijiji bila kuzihakikisha mchipuko wake. Mara kidogo kamsa zilisikika “usiniuwe mi toka nikutoke wa mzee wako, mbona watafuta laana mtoto wewe!”. “Kwani nitaanza kuzipata mimi, we bora nikupeleke jongomeo”. Umati ukazidi kupigwa na butwaa! Maana zile habari za awali za majini na nyoka hazikuonekana kuwa na ukweli wowote kutokana na magombano waliyoyaskia.

Fujo ziliendelea mle ndani, kweli mapambano yalikuwa yamechacha  vyombo vilisikika vikianguka. Watu nao nje hamu na hamumu ziliwazidi kila mayoye yalipozidi. Waliamua wasingeweza kukosa uhondo wote huo, maana milango na madirisha yalikuwa yamefungwa yote na hawakupata kuona lolote. Jagina moja likatokea ili ‘kutafuta suluhu’ na kusukuma watu nyuma, akaanza kuonesha madoido kwa kukaza misuli yake ya mikononi. Watu walimshangilia na kumtia mori, akajawa na ushujaa akaja mbio kwa fujo, na kupita na mlango wa nje kwa bega lake. Naye kweli alikuwa na nguvuze, ule mlango kuuvunja kwa kishindo kimoja ni jambo la kupewa kongole kwa kazi nzuri aliyoifanya.  Naye ‘ushujaa’ ule ulikuja na gharama alianguka kwa kishindo ukumbini na kujipiga na meza. Maskini ya Mungu! Alilia kama kitoto kidogo, bega lilikuwa khalas! tayari lilikuwa limevunjika. Watu wakaanza kumiminika kuingia mle ndani, hata hawakudiriki kumpa usaidizi wa kwanza ‘shujaa’ wao aliyewavunjia mlango. Walimuacha akigaragara chini na kumruka bila hata ya kumjali na lolote. Punde si punde kila mtu alionekana akikimbilia kutoka nje. Mlango ukageuka ‘mdogo’ watu waliparamiana na kusukumana ili wapate nafasi ya kuregea walipotokea. Vilio viliskika tu sana kwa wingi,na wale waliokuwa nje walishindwa kwa nini wenzi wao wanaregea tena kwa kishindo. “Anakuja tayari kashamaliza huko ndani”………………….

 

Author

A freelance writer, journalist, poet and blogger venturing mainly in social and community issues, study and analysis of behaviour and life, and the plight of the under-dogs in the society. 'I feed on human stories.'

Write A Comment