Mwandishi: Mtoto Wa Katama

Fujo ziliendelea mle ndani, kweli mapambano yalikuwa yamechacha vyombo vilisikika vikianguka. Watu nao nje hamu na hamumu ziliwazidi kila mayoye yalipozidi. Waliamua wasingeweza kukosa uhondo wote huo, maana milango na madirisha yalikuwa yamefungwa yote na hawakupata kuona lolote. Jagina moja likatokea ili ‘kutafuta suluhu’ na kusukuma watu nyuma, akaanza kuonesha madoido kwa kukaza misuli yake ya mikononi. Watu walimshangilia na kumtia mori, akajawa na ushujaa akaja mbio kwa fujo, na kupita na mlango wa nje kwa bega lake. Naye kweli alikuwa na nguvuze, ule mlango kuuvunja kwa kishindo kimoja ni jambo la kupewa kongole kwa kazi nzuri aliyoifanya. Naye ‘ushujaa’ ule ulikuja na gharama alianguka kwa kishindo ukumbini na kujipiga na meza. Maskini ya Mungu! Alilia kama kitoto kidogo, bega lilikuwa khalas! tayari lilikuwa limevunjika.

Watu wakaanza kumiminika kuingia mle ndani, hata hawakudiriki kumpa usaidizi wa kwanza ‘shujaa’ wao aliyewavunjia mlango. Walimuacha akigaragara chini na kumruka bila hata ya kumjali na lolote. Punde si punde kila mtu alionekana akikimbilia kutoka nje. Mlango ukageuka ‘mdogo’ watu waliparamiana na kusukumana ili wapate nafasi ya kuregea walipotokea. Vilio viliskika tu sana kwa wingi,na wale waliokuwa nje walishindwa kwa nini wenzi wao wanaregea tena kwa kishindo. “Anakuja tayari kashamaliza huko ndani!”

Kila mtu roho mkononi, kwa mda wa sekunde chache kimya kilitalawa sehemu yote, kama vile wakati ulikuwa umesimamishwa na hakuna kilichosonga. Mara ghafla! Bwanamkubwa Khamisi alichopoka na panga likiwa mkononi, nguo zake zilikuwa zimelowa damu ajabu. Lo! Lile panga lilivyokuwa likitiririka ngeu…..Mmmmhh! kweli asiyekuwa na macho haambiwi tazama. Kwani kuna la zaidi l kuambiwa! Kila mtu tayari alipata picha kamili ya tukio lilojiri. Na kilichobaki  ilikuwa mguu niponye, waliokuwa mbele ya tukio walianza kutawanyika na kusambaratika wakielekea kila upande. Walimpa Khamisi njia, utadhani rais keshaingia mjini, hakuna aliyedhubutu kujifanya shujaa….ili iweje? Kwa kasi ile aliyokuwa akikimbia nayo Khamisi, hakuna ambaye angeweza kumkamata au kudhubutu kumzuia.

Khamisi alitokomea baada ya kupiga vichochoro kadha na kuacha vilio nyuma! Mwili wa ami yake Khamisi alikuwa amelala kifudifudi katika ‘kidimbwi’ cha damu, mwili wake alikuwa amechanjwa chanjwa kwa panga. Teyari mtu keshaenda jongomeo, mwenye roho nyepesi asingeweza kumudu kuangalia mwili ule. Unyama ulioje ule, kila aliyetoka mle ndani alikuwa ameshika kichwa na kuonyesha hali ya kutamaushwa na tukio lile. Mamake Khamisi aligaragara chinina kupiga mayowe, alitoa leso yake na kuanza kuichanachana kwa uchungu. Jirani zake walijaribu kumuauni, lakini wapi waliambulia patupu. Hakuamini katu kisa alichokifanya mwanawe…”Laana gani umeniachia babake Khamisi? Mbona mimi tu” aliomboleza mamake Khamisi kwa fujo, huku machozi yakimdondoka kwa wingi. “ Mama utakufuru Mungu sasa! Ebu! Jitande kwanza na umuogope Mungu” mmoja wa jirani zake alijaribu kumsemesha apunguze maombolezo yake asije akavuka mipaka. Kwa kweli ya Mungu ni mengi, hakuna yeyote aliyedhania matukio kama haya yangetokea, siku ilianza kwa uzuri na utulivu, na jinsi ilivyopinduka kwa ghafla! Kwa muda wote ule watu wakiponda jinsi ya kufanya, kila mtu alijiuliza “ Je Khamisi yuko wapi?……………..

Author

A freelance writer, journalist, poet and blogger venturing mainly in social and community issues, study and analysis of behaviour and life, and the plight of the under-dogs in the society. 'I feed on human stories.'

Write A Comment