Mwandishi: Mtoto wa Katama

Mtaa mzima ulipata habari ya yale yaliyotokea na mamake Khamisi alikuwa mmoja kati ya waliokuwa wakimtafuta Khamisi. Maafisa wa usalama walifika kwenye eneo la tukio, wakauburuza mwili wa marehemu hadi katika gari walilokuja nalo na kuupakia mwili kama vile wamo boharini. Wakakaa kidogo na kujifanya kuuliza maswali wale waliokuwa katika eneo, huku wakitikisa vichwa vyao tu, kama kuonyesha kuwa wanajali sana majibu yaliyokuwa yakitolewa. Kisha hao wakatia gari moto na kuchomoka na maiti.

Mamake Khamisi baada ya kumtafuta kwa muda na kiza kikawa kinaingia bila ya mafanikio yeyote, hakujua afanye nini. Hakuweza kukubali matukio yaliyotokea siku ile, cha zaidi aliomba tu! Siku ingeanza upya, huku machozi yakimdondoka bila kilio chochote. Alikuwa amechoka sana lakini alijiburuta, akaingia jikoni na kujitengenezea kikombe cha chai, mdogo wake Khamisi alikuwa amelala asijue lilotokea. Aliporudi kukaa, alijiuliza Khamisi atakuwa ametokomea wapi. Na wakati ule ilimjia kuwa Khamisi alikimbia na panga mkononi, hivi atakuwa amemwaga damu zaidi huko alikokimbilia au na yeye kapata mbabe aliyemmalizia mbali. Akaanza kugeuka huku na huku, jasho likimtoka, alikumbuka kuwa Khamisi ndiye mwana aliyemtegemea wakumshusha mzigo wa kumlea mdogo wake. Lakini kwa jinsi mambo yalivyotokea, na picha iliyobaki ni aidha Khamisi atauwawa na wanakijiji au aishilie jela milele kwa mauaji ya ami yake. Ndoto zote alizokuwa nazo juu ya mtoto wako zilianza kufifia moja baada ya nyingine. Katika hali ile ya kufikiria na kujilaumu kwa masaibu yake, afua ya Maulana ilimjia na usingizi ukamchukua na kulala chali kama kitoto licha ya masaibu yote.

Mamake Khamisi alipofungua mlango alimwona Bi Sofia amesimama huku amefungata mdomo wake kwa kiganja chake. Maneno yakimtoka kwa kigugumizi “ Ah! Ahhh!, mwenzangu, Innalilahi… waina ilayhi rajiun, sote ni wa Mungu tunaelekea huko huko” alisema kwa masikitiko Bi Sofia. Lakini mamake Khamisi alikuwa kachanganyikiwa, kwa  kweli hakujua anamuongelea nani haswa. “ Hivi bibiye nikuulize, nani katuacha haswa?” aliuliza mamake Khamisi. “Hivi huna habari kabisa mwenzangu, mwanao Khamisi amepatikana pwani huko na wavuvi walioingia alfajiri ya kwanza, kajinyonga kwenye mti ufukweni” Bi Sofia akasema. Hata kabla ya kumaliza maneno yake, mamake Khamisi aliishiwa na nguvu, miguu yake ilishindwa kumueka tisti na akadondoka hadi sakafuni.

Fahamu zilimrudia mamake Khamisi na alikuwa tayari anafarijiwa na wenzake. Uani, majamvi yalikuwa teyari yametandikwa, ile hali ya ‘umatanga’ ilikuwa imeshafika katika nyumba ya mamake Khamisi. Watu walikuwa nao wanamiminika pole pole. Kuna wale waliokuja kutoa pole na kuenda zao na wale walioeka kambi mpaka shughuli nzima itakapomalizika.

Kati ya waombolezaji wale, alitokeo mvuvi mmoja na kumkabidhi Bi Sofia karatasi na kumpa maagizo ampe mamake Khamisi. Karatasi ile ilikuwa ni waraka uliokuwa umeandikwa na Khamisi kabla ya mauti yake, bila kusita mamake Khamisi alifungua na kusoma barua ile ya dhiki japokuwa alikuwa na hamu nayo…” Utakapo soma barua hii mamangu mpendwa itakuwa tayari nimekufa, na la zaidi ungetamani niwe hai ili upate majibu kwa yale niliyoyafanya. Lakini sijutii lolote kwa walimwengu, ila ninahofia Mola wangu atanipokea vipi?. Kukujibu na kukuondeshea makiwa nilifanya hayo yote ili mamangu mzazi uweze kurithi kile alichoacha babangu mzazi, Nishamuondoa nduli aliyezuia haya yote. Nataraji utapata nafasi katika moyo wako na kunisamehe na kama hamna nafasi hiyo, tafadhali niombe kwa Maulana ninapoanza hii safari yangu ya ‘mbinguni’…..

Author

A freelance writer, journalist, poet and blogger venturing mainly in social and community issues, study and analysis of behaviour and life, and the plight of the under-dogs in the society. 'I feed on human stories.'

Write A Comment