Mwandishi: Naima Baghozi

Unaweza kusoma sehemu ya 3: http://lubnah.me.ke/kinyonga-na-tausi-sehemu-ya-3/

Rafiki zake nao wakazidi kutilia mkazo ombi hilo: “Tafadhali Tausi, tafadhali sana, msaidie maskini amesumbuka sana…” wakaendelea hivyo kwa muda kumnasihi Tausi ili akubali. Wakati wote huo Paka alikuwa amejificha juu ya mti karibu kuanguka kwa kujizuia na kicheko maana kila akikaa anastaajabu kwa nini Kinyonga ana lazima ya kujibadilisha rangi yake.

Tausi naye alipoona Kinyonga ananyenyekea sana pamoja na rafiki zake moyo wake ukaingia imani na kuamua: “Sawa nimekubali kumpatia Kinyonga manyoya yangu…lakini sijui kama yatamsaidia…”

Basi hapo hapo Tausi akaanza kujikukuta kukuta na kuyapiga piga mabawa yake na mara mbele ya kikundi hicho manyoya kadhaa yakamtoka na kuanguka chini wote wakafurahi na Tumbiri akasogea na kuanza kuyaokota hayo manyoya. Halafu akamwita Kinyonga: “Sogea karibu na mimi rafiki yangu tuanze kazi ya kukurembesha.” Basi Kinyonga akamsogelea na wenzi wao pia wakajisogeza ili wapate kuona vipi manyoya ya Tausi yataweza kumbadilisha Kinyonga rangi ya mwili wake.

Tumbiri akachukuwa manyoya na kuyaweka juu ya mgongo wa Kinyonga na kuanza kuyasugua kwa ustadi na umakinifu mkubwa. Wote wakawa wanazuia pumzi wakisubiri kwa hamu kuona mabadiliko yatakavyoanza kutokea. Tumbiri aliendelea kufanya ufundi huo kwa makini na subira kubwa mpaka mikono ikaanza kumuuma kwa machofu lakini hakuna hata dalili moja ya mabadiliko iloonekana.

Paka, muda wote huo alikuwa akizuia kicheko chake hapo juu ya mti, hakuweza kujizuia tena. Mara wote waliinua macho waliposikia: “Hahaha-hehehe-hahaha- Nyinyi mnachekesha kweli kweli, hahaha, hehehe! Hata mbavu zinaniuma. Vipi mnaweza kubadilisha tulivyoumbwa? Hahaha…”

Wote walioko chini walikasirika sana na Paka. Kinyonga akamjibu Paka na kumwambia: “We Paka, we endelea tu kunicheka, iko siku hicho kicheko chako kitakukwamia kooni…”

Wakiwa bado wako hapo hapo alitokea mwanadamu akiwa katika matembezi yake. Akaona mkusanyiko wa wanyama hawa utadhani wako kwenye mkutano muhimu, basi akawakurubia na kuwasalimu.
“Habari zenu?” Wakajibu kwa pamoja: “Nzuri.”
“Mbona mumekusanyika? Mna mkutano?”
Akajibu Kinyonga: “Huu mkusanyiko ni kwa ajili yangu na pengine wewe ndie utakaeweza kunisaidia.”
“Ni msaada gani unaouhitaji kwangu?”

Basi Kinyonga akaanza kwa utaratibu kumweleza binadamu shida yake tangu mwanzo hadi mwisho, naye binadamu alisikiliza kwa makini na mwisho akatabasamu tu.

Kinyonga akmuuliza: “Utaweza kunisaidia?”
Mwanadamu akamjibu: “Nimekusikiza kilio chako na nimekufahamu vizuri. Lakini si unafahamu Muumba pekee ndie anaeweza kubadilisha maumbile yetu?”
“Sasa nifanye nini? Mimi nataka sana niwe na mwili wa rangi rangi…”

Mwanadamu akaonyesha ni kama yuko kwenye mawazo mazito. Basi wote walibaki kimya wakisubiri atatoa uamuzi gani. Mwishowe akasema: “Kinyonga, mimi nimefikiri sana na nimeona umwombe Bwana Mola akupatie huo mwili wa rangi rangi unaotaka. Yeye ndie aliekuumba hivyo na yeye peke yake ndie atakayeweza kukubadilisha, basi muombe usiku na mchana na akipenda atakupa hizo rangi uzitakazo kwa mwili wako, sawa?”

Kinyonga na rafiki zake wakakubali kuwa hilo ndilo jawabu la sawa na wote wakamshukuru mwanadamu, akashika njia yake na kuondoka.

Kombamwiko akasema: “Kinyonga, usijali hata sisi kama rafiki zako tutakusaidia kumwomba Bwana Mola, au sivyo wenzangu?” Wote wakajibu: “Naam, sote tuko pamoja.” Paka alipoona bado wanaendelea na wazimu wao aliondoka na kuenda zake akiwaacha na ujinga wao- ndivyo alivyofikiria yeye.

Ibada ya Kinyonga na rafiki zake zikaanza.Usiku na mchana, wakipumzika kidogo tu. Kila kukipambazuka wakimtizama Kinyonga hawaoni mabadiliko yoyote. Lakini hawakuchoka wakaendelea kuomba sana na kwa unyenyekevu. Kwa machofu mengi usiku wa kuamkia siku ya saba usingizi uliwashinda nguvu wakapotelewa na usingizi bila hata ya kuhisi.
Asubuhi na mapema, kulipopambazuka tu na Jua kujitokeza, wa kwanza kuinuka alikuwa Sungura, akawatizama wenzake akawaona wote bado wako usingizini, akajiuliza: “Hivi sote tumeishia kulala bila ya kumwombea rafiki yetu Kinyonga?”

Kisha akageuka huku na huku kumtafuta Kinyonga amelala wapi, akawa hamuoni. Akafanya wasiwasi na kuwaamsha Tumbiri, Tausi na Kombamwiko. Wote wakashtuka kuwa wamelala usiku huu uliopita. Wakauliza: “Kuna nini?”
Sungura akawajibu: “Sote tumepitikiwa na usingizi na hata hatukuweza kumwombea rafiki yetu na sasa hata simuoni, hebu sasa tumtafuteni.” Wakazunguka zunguka wakimtafuta rafiki yao kwa wasiwasi kwani usiku wote walikuwa pamoja.
Hawakufika mbali mara kwa mshangao mkubwa walisimama kwa pamoja midomo yao yote ikiwa wazi isitoke sauti hata moja…

Mbele ya macho yao kulikuwa na jiwe na ubavuni mwake kulikuwa na maua ya rangi ya manjano kijani na nyekundu. Rafiki yao Kinyonga alikuwa amelala usingizi mzito juu ya hilo jiwe mfano ni kama alikuwa anaota jua, asilolijua ni kuwa dua yake imejibiwa. Rafiki zake ndio walikuwa wameona. Kinyonga alikuwa amerembeka kweli. Rangi yake ya mwili iko sawa na rangi zile za maua ubavuni mwake, yaani ngozi yakeimejigawanya rangi za manjano, kijani na nyekundu.
Kwa furaha nyingi hawakuweza kujizuia, kwa shangwe na nderemo na hamu wakamwamsha Kinyonga. Naye Kinyonga akaonyesha ni kama ametoka kwenye usingizi mzito. Akifungua macho yake vizuri akaona rafiki zake wanaruka ruka kwa furaha na kuimba:
“Kinyonga amefaulu, Kinyonga amefaulu, sasa ni mrembo…”

—————————————————————————————————————

Ungana nami katka kipande cha mwisho wa stori hii karibuni in shaa Allah…

Write A Comment

Powered by WordPress