Tag

Kinyonga


Browsing

Mwandishi: Naima Baghozi

Unaweza kusoma sehemu ya 4: https://lubnah.me.ke/kinyonga-na-tausi-sehemu-ya-4/

Mbele ya macho yao kulikuwa na jiwe na ubavuni mwake kulikuwa na maua ya rangi ya manjano kijani na nyekundu. Rafiki yao Kinyonga alikuwa amelala usingizi mzito juu ya hilo jiwe mfano ni kama alikuwa anaota jua, asilolijua ni kuwa dua yake imejibiwa. Rafiki zake ndio walikuwa wameona. Kinyonga alikuwa amerembeka kweli. Rangi yake ya mwili iko sawa na rangi zile za maua ubavuni mwake, yaani ngozi yakeimejigawanya rangi za manjano, kijani na nyekundu.
Kwa furaha nyingi hawakuweza kujizuia, kwa shangwe na nderemo na hamu wakamwamsha Kinyonga. Naye Kinyonga akaonyesha ni kama ametoka kwenye usingizi mzito. Akifungua macho yake vizuri akaona rafiki zake wanaruka ruka kwa furaha na kuimba:
“Kinyonga amefaulu, Kinyonga amefaulu, sasa ni mrembo…”

Akawauliza: “Munasema nini?”
Tumbiri akamjibu: “Umepata ulilotaka, sasa mwili wako umeshakuwa una rangi rangi.”
“Unasema kweli?” Kinyonga akamuuliza akiwa na tabasamu kubwa.
“Naam, hapo ulipo rangi yako iko sawa na maua karibu na wewe.”
Tausi na Kombamwiko pamoja na Sungura wakaongezea: “Ni kweli Kinyonga, hata sisi sote tumeshangaa na urembo wako.”

Mara Kinyonga akafanya kuondoka karibu na hayo maua, zile rangi zikapotea, wenzake wakakatiza furaha zao na kunyamaza kimya, wakamtizama rafiki yao na macho ya kusikitika. Kinyonga akawauliza: “Mbona ghafla furaha imewaishia? Muna nini, na mbona munaniangalia na macho ya huzuni hivyo?”
Aliyemjibu ni Tausi: “Kinyonga hizo rangi tayari zimekupotea.”
“Haiwezekani, sikubali.” Kinyonga akajibu na huku machozi yanamtoka.

Sungura akamwambia Kinyonga asilie naye akajibu: “Nisilie vipi? Baada ya dakika tu kujihisi ni mrembo kwa furaha mulizonionyesha, urembo umenipotea tena.”
Halafu akaondoka na kurudi kwenye jiwe lake na mara zile rangi zilimrudia tena na rafiki zake wakarudi kufurahi tena. Kinyonga akashangaa, na rafiki zake walishangaa zaidi, wakamweleza hayo waliyoyaona. Wakawa hawafahamu ni nini kinachoendelea.

Kinyonga aliwaomba rafiki zake wamtizame akiondoka tena zitafanyika nini. Basi aliondoka hapo na kutembea juu ya mchanga. Rangi za maua ziliondoka na mara alikuwa rangi ya mchanga, alipopita juu ya nyasi akageuka rangi ya kijani. Yaani kila rangi aliyopitia Kinyonga akawa anabadilika kuwa rangi hiyo. Hata alipokuja karibu na Tausi na mkia alikuwa amechanua rangi yake ikawa ya Tausi.

Rafiki zake waliona ni maajabu na kumwelezea yote haya Kinyonga hata akawaambia: “Natamani ningeweza kujiona…” akiwa na wingi wa furaha.
Kombamwiko akasema: “Sungura, wewe ndie ulio na mbio kuliko sisi sote, ni bora ukamfuate Yule mwanadamu, umuelezee kilichotokea na umuombe aje na kioo ili Kinyonga aweze kujiona…”

Sungura akakubali mara moja na hapo hapo akazitoa mbio zake zote mpaka kwa mwanadamu. Njiani alipishana na Paka hata hakumsemesha. Paka akawa anajiuliza mbio hizo Sungura anakwenda wapi? Haikupita muda mrefu akamuona anarudi na mwanadamu akiwa amebeba kioo. Usabasi ukamshika akaamua kuwafuata ili ajue kinachoendelea. Akawafuata kwa kando kando mpaka wakafika sehemu akawaona tena Tausi, Tumbiri na Kombamwiko lakini Kinyonga haonekani. Rafiki zake walikuwa wamemwabia arudi kwenye yale maua ili aonekane na hizo rangi. Basi walipofika walipokuwepo ndio wakamuona Kinyonga na uzuri wake wote. Mwanadamu akamwambia akiwa na mwingi wa tabasamu: “Eh, Kinyonga- umepata ulilotaka sasa nimekuja na kioo ujione ulivyokuwa mrembo.”

Basi akamsimamishia kioo na Kinyonga hakuamini macho yake kwa urembo alouona, akauliza: “Yule ni mimi kweli?” Akajibiwa: “Ni wewe kweli na Sungura amenieleza kuwa unabadilika kila rangi, hebu nionyeshe…”

Kinyonga akaondoka kwenye maua akawa anajionyesha kila sehemu anaposimama anabadilika rangi ya hiyo sehemu. Mwanadamu akamwambia: “Hakika nimekufurahia kwa kupata ulilotaka. Usisahau kumshukuru Bwana Mola kwa kukupatia ulichotaka.”

Kinyonga akamjibu: “Siwezi kusahau, na wewe pia nakushukuru pamoja na hawa rafiki zangu kwa msaada wenu.” Mara akagundua Paka yuko hapo hana la kusema ila mdomo ulikuwa wazi tu, macho yamemkodoka ni kama hayaamini aliyoyaona mbele yake. Kinyonga akamuuliza: “Paka, leo huna ufidhuli wa kusema, si ulituona sisi sote ni wajinga na ukanicheka tu kwa matamanio yangu. Basi leo tunakucheka wewe…

“Hahahaha-hehehehe-hahahaha-hehehehe.” Rafiki zake pamoja na mwanadamu wakamsaidia. “Hahahaha-hehehehe-hahahaha-hehehehe,”

Paka akaondoka kwa unyonge, kichwa na mkia ukiwa chini. Kinyonga na rafiki zake wakaendelea na sherehe zao za kufurahia maisha mapya ya Kinyonga. Yeye mwenyewe aliendelea kuringa ringa, akijigeuza hivi, mara vile. Akaendelea kuishi maisha yake kwa raha mustarehe akijuwa popote anapopita anageuka rangi ya anapopapitia.

Jina la Kinyonga linamaanisha kugeuka geuka na yeye ndivyo alivyo wa kugeuka geuka rangi.

MWISHO.

Mwandishi: Naima Baghozi

Unaweza kusoma sehemu ya 3: https://lubnah.me.ke/kinyonga-na-tausi-sehemu-ya-3/

Rafiki zake nao wakazidi kutilia mkazo ombi hilo: “Tafadhali Tausi, tafadhali sana, msaidie maskini amesumbuka sana…” wakaendelea hivyo kwa muda kumnasihi Tausi ili akubali. Wakati wote huo Paka alikuwa amejificha juu ya mti karibu kuanguka kwa kujizuia na kicheko maana kila akikaa anastaajabu kwa nini Kinyonga ana lazima ya kujibadilisha rangi yake.

Tausi naye alipoona Kinyonga ananyenyekea sana pamoja na rafiki zake moyo wake ukaingia imani na kuamua: “Sawa nimekubali kumpatia Kinyonga manyoya yangu…lakini sijui kama yatamsaidia…”

Basi hapo hapo Tausi akaanza kujikukuta kukuta na kuyapiga piga mabawa yake na mara mbele ya kikundi hicho manyoya kadhaa yakamtoka na kuanguka chini wote wakafurahi na Tumbiri akasogea na kuanza kuyaokota hayo manyoya. Halafu akamwita Kinyonga: “Sogea karibu na mimi rafiki yangu tuanze kazi ya kukurembesha.” Basi Kinyonga akamsogelea na wenzi wao pia wakajisogeza ili wapate kuona vipi manyoya ya Tausi yataweza kumbadilisha Kinyonga rangi ya mwili wake.

Tumbiri akachukuwa manyoya na kuyaweka juu ya mgongo wa Kinyonga na kuanza kuyasugua kwa ustadi na umakinifu mkubwa. Wote wakawa wanazuia pumzi wakisubiri kwa hamu kuona mabadiliko yatakavyoanza kutokea. Tumbiri aliendelea kufanya ufundi huo kwa makini na subira kubwa mpaka mikono ikaanza kumuuma kwa machofu lakini hakuna hata dalili moja ya mabadiliko iloonekana.

Paka, muda wote huo alikuwa akizuia kicheko chake hapo juu ya mti, hakuweza kujizuia tena. Mara wote waliinua macho waliposikia: “Hahaha-hehehe-hahaha- Nyinyi mnachekesha kweli kweli, hahaha, hehehe! Hata mbavu zinaniuma. Vipi mnaweza kubadilisha tulivyoumbwa? Hahaha…”

Wote walioko chini walikasirika sana na Paka. Kinyonga akamjibu Paka na kumwambia: “We Paka, we endelea tu kunicheka, iko siku hicho kicheko chako kitakukwamia kooni…”

Wakiwa bado wako hapo hapo alitokea mwanadamu akiwa katika matembezi yake. Akaona mkusanyiko wa wanyama hawa utadhani wako kwenye mkutano muhimu, basi akawakurubia na kuwasalimu.
“Habari zenu?” Wakajibu kwa pamoja: “Nzuri.”
“Mbona mumekusanyika? Mna mkutano?”
Akajibu Kinyonga: “Huu mkusanyiko ni kwa ajili yangu na pengine wewe ndie utakaeweza kunisaidia.”
“Ni msaada gani unaouhitaji kwangu?”

Basi Kinyonga akaanza kwa utaratibu kumweleza binadamu shida yake tangu mwanzo hadi mwisho, naye binadamu alisikiliza kwa makini na mwisho akatabasamu tu.

Kinyonga akmuuliza: “Utaweza kunisaidia?”
Mwanadamu akamjibu: “Nimekusikiza kilio chako na nimekufahamu vizuri. Lakini si unafahamu Muumba pekee ndie anaeweza kubadilisha maumbile yetu?”
“Sasa nifanye nini? Mimi nataka sana niwe na mwili wa rangi rangi…”

Mwanadamu akaonyesha ni kama yuko kwenye mawazo mazito. Basi wote walibaki kimya wakisubiri atatoa uamuzi gani. Mwishowe akasema: “Kinyonga, mimi nimefikiri sana na nimeona umwombe Bwana Mola akupatie huo mwili wa rangi rangi unaotaka. Yeye ndie aliekuumba hivyo na yeye peke yake ndie atakayeweza kukubadilisha, basi muombe usiku na mchana na akipenda atakupa hizo rangi uzitakazo kwa mwili wako, sawa?”

Kinyonga na rafiki zake wakakubali kuwa hilo ndilo jawabu la sawa na wote wakamshukuru mwanadamu, akashika njia yake na kuondoka.

Kombamwiko akasema: “Kinyonga, usijali hata sisi kama rafiki zako tutakusaidia kumwomba Bwana Mola, au sivyo wenzangu?” Wote wakajibu: “Naam, sote tuko pamoja.” Paka alipoona bado wanaendelea na wazimu wao aliondoka na kuenda zake akiwaacha na ujinga wao- ndivyo alivyofikiria yeye.

Ibada ya Kinyonga na rafiki zake zikaanza.Usiku na mchana, wakipumzika kidogo tu. Kila kukipambazuka wakimtizama Kinyonga hawaoni mabadiliko yoyote. Lakini hawakuchoka wakaendelea kuomba sana na kwa unyenyekevu. Kwa machofu mengi usiku wa kuamkia siku ya saba usingizi uliwashinda nguvu wakapotelewa na usingizi bila hata ya kuhisi.
Asubuhi na mapema, kulipopambazuka tu na Jua kujitokeza, wa kwanza kuinuka alikuwa Sungura, akawatizama wenzake akawaona wote bado wako usingizini, akajiuliza: “Hivi sote tumeishia kulala bila ya kumwombea rafiki yetu Kinyonga?”

Kisha akageuka huku na huku kumtafuta Kinyonga amelala wapi, akawa hamuoni. Akafanya wasiwasi na kuwaamsha Tumbiri, Tausi na Kombamwiko. Wote wakashtuka kuwa wamelala usiku huu uliopita. Wakauliza: “Kuna nini?”
Sungura akawajibu: “Sote tumepitikiwa na usingizi na hata hatukuweza kumwombea rafiki yetu na sasa hata simuoni, hebu sasa tumtafuteni.” Wakazunguka zunguka wakimtafuta rafiki yao kwa wasiwasi kwani usiku wote walikuwa pamoja.
Hawakufika mbali mara kwa mshangao mkubwa walisimama kwa pamoja midomo yao yote ikiwa wazi isitoke sauti hata moja…

Mbele ya macho yao kulikuwa na jiwe na ubavuni mwake kulikuwa na maua ya rangi ya manjano kijani na nyekundu. Rafiki yao Kinyonga alikuwa amelala usingizi mzito juu ya hilo jiwe mfano ni kama alikuwa anaota jua, asilolijua ni kuwa dua yake imejibiwa. Rafiki zake ndio walikuwa wameona. Kinyonga alikuwa amerembeka kweli. Rangi yake ya mwili iko sawa na rangi zile za maua ubavuni mwake, yaani ngozi yakeimejigawanya rangi za manjano, kijani na nyekundu.
Kwa furaha nyingi hawakuweza kujizuia, kwa shangwe na nderemo na hamu wakamwamsha Kinyonga. Naye Kinyonga akaonyesha ni kama ametoka kwenye usingizi mzito. Akifungua macho yake vizuri akaona rafiki zake wanaruka ruka kwa furaha na kuimba:
“Kinyonga amefaulu, Kinyonga amefaulu, sasa ni mrembo…”

—————————————————————————————————————

Ungana nami katka kipande cha mwisho wa stori hii karibuni in shaa Allah…

Mwandishi: Naima Baghozi

Unaweza kusoma sehemu ya 2: https://lubnah.me.ke/kinyonga-na-tausi-sehemu-ya-2/

Maskini Kinyonga akajitizama na kuona michirizi ya rangi iliyokuwa ikitiririka kutoka mwilini mwake. Moyo ulimuuma na machozi kumbubujika buji buji akiuona urembo wake huooo unamtoka. Kombamwiko alimbembeleza sana na kujaribu kila njia ya kumnyamazisha lakini wapi…ndio mwanzo Kinyonga alikuwa anazidisha kilio mpaka mwisho Kombamwiko akamwambia: “Sikiza rafiki yangu, usilie sana. Naona ni bora urudi kwa Tumbiri umuombe akusaidie tena na sasa umeshajua ukiona mvua ukimbie wala usikaribie maji yoyote, sawa?”

Kinyonga hapo akapata moyo kidogo na kuamua kufanya hivyo. “Shukrani sana Kombamwiko kwa nasiha yako nzuri, naona ndivyo nitakavyofanya. Kwaheri kwa sasa , wacha nianze safari ya kwenda kwa Tumbiri , tutaonana.”
“Kwaheri ya kuonana na nakutakia kila la heri.”

Kinyonga akashika njia ya kurudia huko huko alikotoka. Safari yenyewe ilikuwa si fupi lakini aliamua kwenda hivyo hivyo maana lengo lake ni kubadili rangi ya mwili wake. Basi akaenda kwa mwendo wa kasi kadiri alivyoweza mpaka alipofika nusu ya njia akakutana na Sungura katika shughuli zake za kuchimba chimba akijitafutia chakula.

Akamsalimia kwa furaha : “Aah! Sungura rafiki yangu, habari za siku nyingi?” Sungura akamjibu : “ Nzuri Kinyonga. Ni kweli tumepotezana kwa muda mrefu sana. Hivi unaelekea wapi?”
“Kwa vile nimekuona wewe pengine sina haja ya kwenda nilikokuwa ninaenda.”
“kwani ulikuwa unaenda wapi? Na mimi ninaweza kukusaidia vipi?” Sungura akauliza tena.
“Wewe Sungura, sote tunakufahamu kwa ujanja na werevu wako ndio nimeona wewe utaweza kunipa ushauri bora nipate lengo langu.” Basi Kinyonga akaendelea na kumweleza kisa chake tangu mwanzo hadi mwisho.
Sungura akamuuliza: “Kwa ufupi unataka uwe na rangi kama za Tausi au sivyo?”
“Ndivyo,” akajibu Kinyonga.
Sungura akamwambia : “Mimi naona bora uende kwa Tausi umuombe akutolee manyoya mawili matatu hivi ujifutilie juu ya mwili wako na pengine utakuwa na rangi kama yeye.”
Kinyonga akashangaa sana na na huku akiwaza vipi tangu mwanzo hakufikiria hivyo. “Aah! Sungura si nimesema wewe u mwerevu sana, utakuja na mimi unisaidie kumwomba Tausi?”

Sungura akakubali kurudi naye. Walipotaka kuondoka walimuona Tumbiri anakuja. Alipowasili aliwasalimia na kuuliza kilichokuwa kinaendelea na sababu ya Kinyonga kutokuwa na rangi. Basi Kinyonga akamweleza kile kilichotokea na walichokuwa wananuia kufanya yeye na Sungura.

Tumbiri akamuonea huruma na kumwambia : “Usihuzunike rafiki yangu hata mimi nitakwenda na nyinyi tukamtaradhie kwa vizuri Tausi ili akupatie hayo manyoya yake.”

Basi safari ya watatu hao ikaanza kwa mwendo wa haraka. Mara njiani wakamkuta Paka, nae aliona mbio walizokuwa wanakuja nazo. Mwanzoni alikuwa hajamwona Kinyonga lakini walipomkaribia akamuona Kinyonga bila ya rangi rangi zake akaanza na kicheko chake: “Hahahaha, hehehehe Kinyonga hahaha ziwapi rangi zako?” Kinyonga kwa hasira akawaambia Tumbiri na Sungura: “Mwacheni huyu Paka na ujinga wake. Twendeni zetu.” Wakaondoka kwa haraka. Paka akaamua kuwafuata nyuma nyuma ajue wanakwenda wapi na wanakwenda kufanya nini.

Bila ya kujua kama Paka anawafuata kisirisiri, Kinyonga na maswahibu zake waliendelea na safari yao ya kwenda kwa Tausi. Kabla ya kuwasili kwa Tausi wakampata Kombamwiko mbele yao. Akamuuliza Kinyonga: “Mbona rafiki yangu umerudi hivyo hivyo bila kupaka rangi zako?”

Kinyonga akamweleza nini wameamua kufanya. Basi Kombamwiko akaamua kuwafuata. Msafara ukaendelea mpaka kwa Tausi. Tausi kama kawaida alikuwa akizunguka zunguka kwa maringo katika bustani. Mara akauona msafara unamwingilia wa Tumbiri, Sungura, Kinyonga na Kombamwiko.

Asiyemuona alikuwa ni Paka maana alikuwa amejificha wasimuone. Hamu yake nikutaka kujua kuna sababu gani ya wote hawa kuja mpaka kwa Tausi. Tausi mwenyewe aliona ajabu kuwaona wote hawa pamoja kwani kwa kawaida kila mmoja huwa kivyake. Akaona bora awaulize: “Habari zenu? Muna nini leo, mbona mmeandamana kuja kwangu?”
Akajibu Sungura: “Nzuri Tausi. Sisi tumejikusanya kwako na ombi dogo tukutaradhie kama utaweza kutusaidia. Tausi akashangaa huku akiwaza ombi gani hilo lililowafanya hawa wote kujikusanya na kuja kwake. Akaamua kutaka kujuwa: “Ombi gani hilo? Hebu niambieni na nikiweza nitakusaidieni.”

Tumbiri akapata moyo kidogo akasongea mbele na kusema: “Tausi, wewe unajua vizuri vipi Kinyonga anatamani kuwa na mwili wa rangi rangi kama wewe sivyo?”
Tausi akajibu: “Naam ni kweli, kwa hivyo munataka mimi nifanye nini?”

Kinyonga akajisogeza mwenyewe na kumweleza mambo yote yaliyojiri tangu alipoachana na yeye mpaka muda ule walipofika kwake. Akamalizia na kusema:
“Sasa nakuomba unisaidie na manyoya yako mawili matatu ili nijipake mwilini mwangu na pengine nitakuwa na rangi nzuri kama zako.”

Rafiki zake nao wakazidi kutilia mkazo ombi hilo: “Tafadhali Tausi, tafadhali sana, msaidie maskini amesumbuka sana…” wakaendelea hivyo kwa muda kumnasihi Tausi ili akubali. Wakati wote huo Paka alikuwa amejificha juu ya mti karibu kuanguka kwa kujizuia na kicheko maana kila akikaa anastaajabu kwa nini Kinyonga ana lazima ya kujibadilisha rangi yake.

Tausi naye alipoona Kinyonga ananyenyekea sana pamoja na rafiki zake moyo wake ukaingia imani na kuamua: “Sawa nimekubali kumpatia Kinyonga manyoya yangu…lakini sijui kama yatamsaidia…”

————————————————————————————————————-

Itaendelea karibuni in shaa Allah 🙂

Mwandishi: Naima Baghozi

Unaweza kusoma sehemu ya kwanza ya hekaya hii: https://lubnah.me.ke/kinyonga-na-tausi-sehemu-ya-1/

 

“HAHAHA HAHAHA HEHEHE….” Aliangua kicheko kile huku akiwa chali mara akijipindua hivi na vile maana aliona ajabu kuwa Kinyonga aliamini ataweza kujigeuza rangi ya mwili wake.

Kinyonga alipoona namna anavyocheka paka kwa stihizai alikasirika na kuondoka huku akilini akijiambia, “Nitamwonesha huyu Paka kuwa naweza kujigeuza!”

Basi akaendelea na safari yake mpaka akatokezea pahala penye miti kiasi na hapo akamuona Tumbiri akirukaruka kutoka mti mmoja hadi mwingine katika hali ya kucheza cheza . Alipomuona Kinyonga akasita katika michezo yake.

“Kinyonga, habari ya siku nyingi? Kitambo sijakuona, ulikuwa wapi?” Akajibu Kinyonga : “Nilikuwa huko mbali kwenye boma la Tausi.” Tumbiri akamuuliza : “Ulikuwa unafanya nini muda wote huo?” Nae akamjibu: “Nilikuwa nikiushangilia na kuufwatilia uzuri wa rangi zake na hasa anapochanua mkia wake. Zile rangi zake zinanipendezea sana mpaka nimetamani kuwa nazo. Je, unaweza kunishauri vipi nitaweza kuzipata rangi hizo nzuri mwilini mwangu?”

Tumbiri akamtazama Kinyonga bila kumwambia kitu kwanza kisha akamwabia: “Hmm! Subiri nifikiri kidogo .” Wakaketi kimya kidogo huku Tumbiri akijikuna kichwa akiwa mwenye bahari ya mawazo. Mara akaruka ghafla juu na chini akimwambia Kinyonga kuwa ameshapata jawabu la suala lake. Kinyonga nae akainua uso wake kwa bashasha na furaha nyingi akimtaka Tumbiri amjibu kwa haraka. “Niambie rafiki yangu, wewe ndiye rafiki yangu wa kikweli kweli.” Tumbiri akamnyamazisha kwa kumwambia: “Unaona giza limeanza kuingia , bora tulale, tupumzike hadi asubuhi. Maoni yangu ni kuwa tukusanye maua ya kila rangi kama mekundu , manjano, zambarau, kijani na kadhalika. Kisha tuyatie maji kidogo na kuyaponda ponda mpaka yatoe rangi, hiyo rangi ukijipaka mwilini mwako kila sehemu rangi tofauti utakuwa mrembo kama Tausi. Unaionaje fikra yangu?”

Kinyonga alishindwa kuficha furaha yake na akajibu kwa wingi wa bashasha: “Maoni yako ni mazuri sana na naona ni njia nzuri kabisa. Haya tulale basi ili tuweze kurauka.”

Basi kila mmoja akashika upande wake na kulala lakini Kinyonga kwa ile hamu aliyokuwa hakuweza kulala vizuri maana aliona hata asubuhi haitofika…

Hata kabla ya kupambazuka vizuri alikuwa tayari kuianza hiyo shughuli ya kutafuta maua . Kwa vishindo vyake na kufurukuta kwake Tumbiri akainuka nae kwa kughasika akamuuliza Kinyonga : “Mbona unafanya vishindo mpaka umenikatiza usingizi wangu? Mwenyewe nilkuwa ninaota ndoto nzuri …”

“Ndoto gani ya saa hizi? Huoni asubuhi imeshafika? Inuka tukatafute hayo maua.” Tumbiri akajibu: “Wewe hata umelala? Sasa hata mwangaza haujatoka. Sasa tutaona nini hivi? Tusubiri kidogo zaidi.” Basi Kinyonga akawa hana budi ila kusubiri mwangaza utokeze vizuri maana alijua bila ya usaidizi wa Tumbiri hatoweza kufanya lolote.

Akawa anaenda mbele akirudi nyuma huku akijipatia vidudu akijilia. Mwangaza ulipojitokeza vizuri Tumbiri akamwambia:”Haya rafiki yangu wakati umewadia. Twende tukakusanye maua tuje tuanze kazi.”

Kinyonga hakuweza kuficha hamu yake akasema: “Haya twende zetu.” Wakaondoka na kabla ya kufika mbali wakakiona kiwanja kilichopambika kwa maua ya rangi ainati, yaani kila rangi waliotaka waliipata hapo. Nao hawakuchelewa kuanza kukusanya. Kinyonga alikuwa amebahatika kwani Tumbiri alikuwa na mikon kama ya binadamu kwa hivyo kazi ilifanyika vizuri. Muda si muda Tumbiri akasema: “ninaona haya tuliyoyakusanya yanatosha. Twende zetu.”

Wakarudi maskani yao. Tumbiri akachukua maji kidogo na jiwe na kuanza kuyaponda ponda yale maua kila rangi kivyake. Yalipotoa rangi alimwambia Kinyonga “Haya rafiki yangu rangi zote ziko tayari njoo nikupake upate kurembeka.”

Kinyonga akasogea mpaka alipo Tumbiri naye akaanza kumpaka rangi moja baada ya nyingine yaani kijani kisha nyekundu kisha zambarau kisha manjano na rangi nyinginezo kwa ustadi kabisa. Alipomaliza akamwambia : “Eeh Kinyonga umependeza kweli. Sasa sogea ukae penye jua upate kukauka vizuri. Kinyonga akaenda palipo na jua huku akiuliza : “Nimependeza kweli?” Tumbiri akamjibu kuwa kila atakayemwona angemwonea wivu.

Basi akajituliza juani na kwa sababu usiku hakulala vizuri akapatwa na usingizi. Ni kama alikuwa akiota jua.Aliposhtuka ilikuwa imeshafika adhuhuri. Akamuaga Tumbiri kuwa anaaondoka: “Mimi sasa ninarudi nikamwonyeshe paka aliyekuwa akinicheka na kombamwiko aliyesema sitoweza geuka na hasa huyo tausi aliyenidharau.”

Tumbiri akajaribu kunasihi abaki nae zaidi kidogo lakini alikataa kata kata . “Samahani rafiki yangu lakini hujui ile hamu niliyo nayo kuwafikia hao walionidharau. Tutaonana siku nyingine na asante sana kwa usaidizi wako rafiki yangu, wewe peke yako ndiye uliyesimama na mimi.Haya kwaheri ya kuonana…”

“Kwaheri ya kuonana.” Tumbiri akamjibu.

Kinyonga akaanza safari yake ya kurudi maskani yake anapoishi na Tausi. Akatembea kwa muda mrefu, mara akamwona Paka ,akamwita: “Paka, Paka wajidai hunioni. Niangalie, niangalie uone urembo wangu.”  Huku akijigeuza hivi na vile ili aone rangi zake tofauti tofauti. Akaendelea: “Mbona sasa hunicheki, nicheke kama ulivyonicheka mwanzo. Hahahaha-hehehehe.” Akimuigiza vile alivyomcheka mara ya kwanza. Paka akamjibu kwa mshangao: “Aah! Kinyonga, huyu ni wewe kweli?” huku akimzunguka zunguka. Kinyonga hakumjibu kitu. Aliondoka tu na kwenda zake akimwacha Paka kinywa wazi.

Basi safari ikaendelea njia nzima maringo yakimzidi na pia akitafakari vile alivyomuacha Paka na mshangao. Kinyonga akaendelea mpaka alipokutana na kombamwiko. Naye pia hakusita  kuona maajabu ya mabadilko ya Kinyonga ,akamuuliza: “Kinyonga, ni wewe au ni macho yangu? Umekuwa mrembo kweli. Umefanya nini hadi kupata rangi hizo nzuri nzuri mwilini mwako?”

Kinyonga akamjibu: “Sikukosa wa kunisaidia, ingawaje nyinyi huku mlikataa kabisa.”

“Sio tulikataa nawe, ni kuwa hatukujua tukusaidie vipi. Niambie basi ulimpata nani wa kukusaidia?” Kwa maringo zaidi kinyonga akaanza kumwelezea namna Tumbiri alivyomsaidia tangu mwanzo hadi mwisho. Alipomaliza akawa anamuaga Kombamwiko hamu yake kubwa ni kumfikia Tausi ili auone urembo wake. Mara kwa ghafla kukateremka mvua , mvua iliyokua haitarajiwi. Kombamwiko mbio mbio akaingia kwenye kipango chake ili kujikinga na mvua na Kinyonga maskini akawa anahangaika hajui ajifiche wapi, mwisho akapata majani ya mkungu yaliokuwa yameanguka chini akajibarizi hapo.

Haikuchukuwa muda mrefu, mvua kama ilivyoshuka kwa ghafla na pia ikasimama kwa ghafla na pia ikasimama kwa ghafla. Kukawa kimya kwa muda mfupi.

Kombamwiko akatoka makaoni pake na kuangalia Kinyonga alikokuwepo huku akimuita, : “ Kinyonga, Kinyonga..,uko wapi?”

Kwa utaratibu Kinyonga akajitokeza na kujibu “ Mimi niko hapa..” Akanyamaza ghafla kwa kumuona jinsi Kombamwiko alivyokuwa akimtizama kwa sura ya huzuni kubwa.

“Mbona unaniangalia hivyo?” Akauliza. Jawabu alilopata ni: “Urembo umeshakutoka rafiki yangu …”

“Ukimaanisha nini?” Kinyonga akashangaa. Kombamwiko akauliza: “Umesahau kuwa si maumbile yako bali ni rangi tu ulizojipaka?”

“Kwa hivyo…?” Kinyonga akarudi kuuliza. “Kwa hivyo ile mvua iliyokupiga imebakisha michirizi ya rangi tu mwilini mwako tena zimechanganyika changanyika. Hebu tizama chini yako huoni mitiririko ya rangi?”Maskini Kinyonga akajitizama na kuona michirizi ya rangi iliyokuwa ikitiririka kutoka mwilini mwake. Moyo ulimuuma na machozi kumbubujika buji buji akiuona urembo wake huoooo unamtoka.


Itaendelea karibuni…

 

Mwandishi: Naima Baghozi

Tausi alikuwa anazunguka zunguka katika bustani kwa maringo, akitembea na mwendo wa aste aste, akiuchanua mkia wake kama ua kubwa. Kwa hakika yeye ni ndege mrembo sana na hasa pale anapochanua mkia wake. Wakati wote huo alipokuwa akiringa ringa, hakujuwa kuwa alikuwa anafuatwa na macho asiyoyaona. Anapokwenda au anapozunguka, macho yale yalikuwa yakiuandama kwa matamanio makubwa. Macho yenyewe makubwa ya kiasi kwa hivyo yalikuwa hayapitwi na jambo lolote. Mwenye macho mashuhuri hayo alikuwa ni kinyonga. Kinyonga wakati huo alikuwa na rangi moja tu ya rangi ya kunde. Lakini kinyonga hakuridhika na rangi yake basi alibaki kummezea mate Tausi kwa uzuri wake alompa Mola. Alikuwa akitamani sana kama na yeye angeweza kuwa na rangi nzuri nzuri kwenye mwili wake ili avutie kama tausi.

Kila uchao yeye alikuwa akikaa juu ya ukuta kimya na kumtazama tausi anavyojishaua na huku akili yake ikimuenda kama saa kwa mawazo. Alikuwa akipanga na kupangua vipi na yeye ataweza kuwa mrembo kama tausi. Mwisho akaamua bora amwulize tausi mwenyewe. Akamwita kwa sauti ya unyenyekevu,

“Tausi…”

“Naam kinyonga, unasemaje?”

“Mimi kila siku sina kazi ya kufanya ila kukaa hapa kwenye ukuta na kukuangalia unavyotembea kwa maringo huku na huku, hasa ukichanua mkia wako,” Kinyonga akasema.

“Na wewe hupendi?” Tausi akamwuliza.

“Sio hivyo rafiki yangu. Mimi nilikuwa napendezewa na hizo rangi zako nzuri na natamani na mimi ningeweza kuwa na rangi kama hizo. Si bora ungenipa na mimi hiyo siri yako ili na mimi niwe mzuri kama wewe?”

Tausi akacheka sana, “Ha ha ha Ha ha ha” mpaka akawa hawezi kujizuia. Kinyonga akashangazwa na hali hii ya tausi mwishowe akamuuliza akamuuliza, “ni kitu gani kimekuchekesha namna hiyo?”

Tausi kwa taabu akajizuia huko kucheka kwake na kumjibu, “Umenichekesha rafiki yangu kwa sababu vipi utapata uzuri kama wangu au siri gani hiyo nikupe uweze kujibadilisha? Kwani mimi sikujiumba mwenyewe kuwa hivi…”

Kinyonga akamkatiza maneno kwa kumwambia, “Sawa kama hutaki kunisaidia, wewe ringa tu, mimi nitatafuta njia mwenyewe.” Tausi akamtizama kwa mshangao akiwaza je huyu Kinyonga ataweza vipi kujigeuza?  Kinyonga akaondoka na huzuni na masikitiko akimwacha Tausi na fikra.

Mapambazuko ya siku ya pili na mapema yalimpata Kinyonga tayari yuko njiani kujitafutia njia ya kujigeuza na ndio akakutana na Kombomwiko.

“Habari ya asubuhi Mende.”

“Nzuri sana Kinyonga. Je mbona na asubuhi mapema leo? Unaelekea wapi?”

“Ah rafiki yangu pengine hata wewe utaweza kunisaidia.”

“Niambie rafiki yangu, nikiweza nitakusaidia,” akajibu Kombomwiko.

Basi Kinyonga akaendelea, “Mimi natamani sana niwe na rangi mwilini kama vile Tausi na sijui nifanye vipi hata niweze kupata rangi hizo. Je unaweza kunisaidia kimawazo?”

Kombomwiko akamjibu,“Ah! Kwani rangi yako ina nini? Si mimi pia niko na rangi moja mwili mzima na nimeridhika nayo? Hivi ndivyo tulivyoumbwa.”

Kinyonga akaona hapa hatopata msaada wowote akamwambia Kombomwiko, “Basi wewe bakia hivyo hivyo, mimi nitaendelea kutafuta njia ya kuweza kujigeuza rangi niwe kama Tausi. Kwaheri.” Akashika njia yake na kumwacha Kombomwiko na wazo kama za Tausi; je ni vipi ataweza Kinyonga kujigeuza rangi ya mwili wake?

 

male-or-female-chameleon-1

Kinyonga akaendelea na safari yake na baada ya muda akakutana na paka akamtangulizia salamu.

“Paka hujambo?”

“Sijambo Kinyonga. Leo mbona uko mbali huku na makao yako ya kawaida?” Paka akauliza.

“Niko njiani nikitafuta namna ya kujigeuza niwe na rangi nzuri nzuri kama Tausi…”

Hata kabla hajamaliza matamshi yake, Paka akamkatiza na kicheko cha ajabu.

“HAHAHA HAHAHA HEHEHE….” Aliangua kicheko kile huku akiwa chali mara akijipindua hivi na vile maana aliona ajabu kuwa Kinyonga aliamini ataweza kujigeuza rangi ya mwili wake.

Kinyonga alipoona namna anavyocheka paka kwa stihizai alikasirika na kuondoka huku akilini akijiambia, “Nitamwonesha huyu Paka kuwa naweza kujigeuza!”…..


Je Kinyonga ataweza kubadilisha rangi ya mwili wake? Ungana na mimi wakati ujao Mungu akipenda tufatilie hadithi hii!