Mwandishi: Naima Baghozi

Unaweza kusoma sehemu ya 4: http://lubnah.me.ke/kinyonga-na-tausi-sehemu-ya-4/

Mbele ya macho yao kulikuwa na jiwe na ubavuni mwake kulikuwa na maua ya rangi ya manjano kijani na nyekundu. Rafiki yao Kinyonga alikuwa amelala usingizi mzito juu ya hilo jiwe mfano ni kama alikuwa anaota jua, asilolijua ni kuwa dua yake imejibiwa. Rafiki zake ndio walikuwa wameona. Kinyonga alikuwa amerembeka kweli. Rangi yake ya mwili iko sawa na rangi zile za maua ubavuni mwake, yaani ngozi yakeimejigawanya rangi za manjano, kijani na nyekundu.
Kwa furaha nyingi hawakuweza kujizuia, kwa shangwe na nderemo na hamu wakamwamsha Kinyonga. Naye Kinyonga akaonyesha ni kama ametoka kwenye usingizi mzito. Akifungua macho yake vizuri akaona rafiki zake wanaruka ruka kwa furaha na kuimba:
“Kinyonga amefaulu, Kinyonga amefaulu, sasa ni mrembo…”

Akawauliza: “Munasema nini?”
Tumbiri akamjibu: “Umepata ulilotaka, sasa mwili wako umeshakuwa una rangi rangi.”
“Unasema kweli?” Kinyonga akamuuliza akiwa na tabasamu kubwa.
“Naam, hapo ulipo rangi yako iko sawa na maua karibu na wewe.”
Tausi na Kombamwiko pamoja na Sungura wakaongezea: “Ni kweli Kinyonga, hata sisi sote tumeshangaa na urembo wako.”

Mara Kinyonga akafanya kuondoka karibu na hayo maua, zile rangi zikapotea, wenzake wakakatiza furaha zao na kunyamaza kimya, wakamtizama rafiki yao na macho ya kusikitika. Kinyonga akawauliza: “Mbona ghafla furaha imewaishia? Muna nini, na mbona munaniangalia na macho ya huzuni hivyo?”
Aliyemjibu ni Tausi: “Kinyonga hizo rangi tayari zimekupotea.”
“Haiwezekani, sikubali.” Kinyonga akajibu na huku machozi yanamtoka.

Sungura akamwambia Kinyonga asilie naye akajibu: “Nisilie vipi? Baada ya dakika tu kujihisi ni mrembo kwa furaha mulizonionyesha, urembo umenipotea tena.”
Halafu akaondoka na kurudi kwenye jiwe lake na mara zile rangi zilimrudia tena na rafiki zake wakarudi kufurahi tena. Kinyonga akashangaa, na rafiki zake walishangaa zaidi, wakamweleza hayo waliyoyaona. Wakawa hawafahamu ni nini kinachoendelea.

Kinyonga aliwaomba rafiki zake wamtizame akiondoka tena zitafanyika nini. Basi aliondoka hapo na kutembea juu ya mchanga. Rangi za maua ziliondoka na mara alikuwa rangi ya mchanga, alipopita juu ya nyasi akageuka rangi ya kijani. Yaani kila rangi aliyopitia Kinyonga akawa anabadilika kuwa rangi hiyo. Hata alipokuja karibu na Tausi na mkia alikuwa amechanua rangi yake ikawa ya Tausi.

Rafiki zake waliona ni maajabu na kumwelezea yote haya Kinyonga hata akawaambia: “Natamani ningeweza kujiona…” akiwa na wingi wa furaha.
Kombamwiko akasema: “Sungura, wewe ndie ulio na mbio kuliko sisi sote, ni bora ukamfuate Yule mwanadamu, umuelezee kilichotokea na umuombe aje na kioo ili Kinyonga aweze kujiona…”

Sungura akakubali mara moja na hapo hapo akazitoa mbio zake zote mpaka kwa mwanadamu. Njiani alipishana na Paka hata hakumsemesha. Paka akawa anajiuliza mbio hizo Sungura anakwenda wapi? Haikupita muda mrefu akamuona anarudi na mwanadamu akiwa amebeba kioo. Usabasi ukamshika akaamua kuwafuata ili ajue kinachoendelea. Akawafuata kwa kando kando mpaka wakafika sehemu akawaona tena Tausi, Tumbiri na Kombamwiko lakini Kinyonga haonekani. Rafiki zake walikuwa wamemwabia arudi kwenye yale maua ili aonekane na hizo rangi. Basi walipofika walipokuwepo ndio wakamuona Kinyonga na uzuri wake wote. Mwanadamu akamwambia akiwa na mwingi wa tabasamu: “Eh, Kinyonga- umepata ulilotaka sasa nimekuja na kioo ujione ulivyokuwa mrembo.”

Basi akamsimamishia kioo na Kinyonga hakuamini macho yake kwa urembo alouona, akauliza: “Yule ni mimi kweli?” Akajibiwa: “Ni wewe kweli na Sungura amenieleza kuwa unabadilika kila rangi, hebu nionyeshe…”

Kinyonga akaondoka kwenye maua akawa anajionyesha kila sehemu anaposimama anabadilika rangi ya hiyo sehemu. Mwanadamu akamwambia: “Hakika nimekufurahia kwa kupata ulilotaka. Usisahau kumshukuru Bwana Mola kwa kukupatia ulichotaka.”

Kinyonga akamjibu: “Siwezi kusahau, na wewe pia nakushukuru pamoja na hawa rafiki zangu kwa msaada wenu.” Mara akagundua Paka yuko hapo hana la kusema ila mdomo ulikuwa wazi tu, macho yamemkodoka ni kama hayaamini aliyoyaona mbele yake. Kinyonga akamuuliza: “Paka, leo huna ufidhuli wa kusema, si ulituona sisi sote ni wajinga na ukanicheka tu kwa matamanio yangu. Basi leo tunakucheka wewe…

“Hahahaha-hehehehe-hahahaha-hehehehe.” Rafiki zake pamoja na mwanadamu wakamsaidia. “Hahahaha-hehehehe-hahahaha-hehehehe,”

Paka akaondoka kwa unyonge, kichwa na mkia ukiwa chini. Kinyonga na rafiki zake wakaendelea na sherehe zao za kufurahia maisha mapya ya Kinyonga. Yeye mwenyewe aliendelea kuringa ringa, akijigeuza hivi, mara vile. Akaendelea kuishi maisha yake kwa raha mustarehe akijuwa popote anapopita anageuka rangi ya anapopapitia.

Jina la Kinyonga linamaanisha kugeuka geuka na yeye ndivyo alivyo wa kugeuka geuka rangi.

MWISHO.

Write A Comment

Powered by WordPress